Saturday, August 18, 2012

NI FILAMU YA KISA CHA KANUMBA?

Miss Tanzania No. 3, 2009, Julieth William Lugembe nyota wa filamu mpya ya "Sister Julieth"
Miss Tanzania No. 3, 2009, Julieth William Lugembe (kushoto) na Sylvia Shally Miss TZ No.4 2009 ambao wamecheza filamu mpya ya "Sister Julieth"

MISS Tanzania Na.3 wa mwaka 2009, Julieth William amemshirikisha mrembo mwenzake aliyeshika Na.4 mwaka huo, Sylvia Shally, katika filamu mpya inayokwenda kwa jina la "Sister Julieth".

Filamu hiyo ambayo iko katika hatua ya uhariri inaelezea kisa cha kijana ambaye anatuhumiwa kumuua rafikiye wa kike wakati wakiwa peke yao chumbani na kesi mahakamani inamuelemea kijana huyo.

Sister Julieth, nafasi ambayo inachezwa na Sylvia, anakuja kama mzimu na kumtetea kijana huyo, ambaye anakumbana na upinzani mkali kutoka kwa mawakili wa upande wa mashitaka.

Mrembo huyo aliyegeukia katika uigizaji, alisema hii ni filamu yake ya kwanza kucheza, kama ilivyo kwa Sylvia na kwamba ameitunga yeye mwenyewe.

Baada ya mwandishi kuhoji kama filamu hiyo inahusiana na tukio la marehemu Steven Kanumba aliyefariki wakiwa peke yao chumbani na muigizaji Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, aling'aka: "Aaah hapana. Hata kidogo. Ni kisa tofauti kabisa. Ni kisa kinachouhusisha mzimu unaokuja duniani kutoa ushahidi.

"Ni kati ya filamu za hisia kali. Iko katika hatua ya uhariri na wakati wowote itatoka."

Alisema katika filamu hiyo amewashirikisha pia wasanii wengine maarufu akiwamo Dude.

Katika shindano la Miss Tanzania 2009 ambalo Julieth alishika Na.3, Miriam Gerald aliibuka mshindi wa kwanza, Beatrice Lukindo alikuwa wa pili wakati nafasi ya nne ilishikwa na Sylvia na Sia Ndaskoi alikamilisha Top 5.

No comments:

Post a Comment