Friday, August 3, 2012

NGASSA KUTAMBULISHWA SIMBA LEO

Mrisho Ngassa

Akibusu jezi ya Yanga..... sababu iliyomfanya akaondoka Azam
KLABU ya Simba inatarajia kumtambulisha winga wake mpya, Mrisho Ngassa iliyemsajili kwa mkopo wa msimu mmoja kutokea katika klabu ya Azam FC.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Goffrey Nyange 'Kaburu' ambaye alipambana kwa kila awezalo kuhakikisha winga huyo wa timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, anatua Msimbazi, alisema kuwa wanajipanga kumtambusha Ngassa baada ya kukamilisha uhamisho wake. Simba imelipa Sh. milioni 25 kwa Azam.

Awali, Ngassa, nyota wa zamani wa mahasimu wa jadi, Yanga, alisema hayuko tayari kuuzwa kama nyanya kutoka Azam kwenda Simba, lakini baada ya uongozi wa Simba kuzungumza naye jana, nyota huyo alisema amekubali kujiunga na Wekundu wa Msimbazi.

Ngassa aliisifu klabu ya Simba kwamba si miongoni mwa zenye tabia ya kufukuza fukuza wachezaji na kwamba anaamini ataipa mafanikio baada ya kutolewa mapema dhidi ya Azam katika robo fainali ya Kombe la Kagame lililomalizika wiki iliyopita kwa mahasimu Yanga kutwaa ubingwa wa pili mfululizo kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

"Leo nimedmalizana na klabu ya Azam, nimefikia makubaliano na klabu ya Simba. Kama kuna tatizo lolote lilitokea Azam naomba wanisamehe. Nawaomba mashabiki wa Simba wanipokee kwa maendeleo ya klabu," alisema Ngassa jana baada ya kumalizana na uongozi wa Simba.

Rafiki wa karibu wa mchezaji huyo, ambaye kuondoka kwake Azam kumefuatia kuvaa na kuibusu jezi ya timu ya Yanga, alisema kuwa uongozi wa Simba umefanikiwa kumshawishi Ngassa atue wa wapinzani baada ya kumuahidi kumpa Sh. milioni 12 pamoja na gari na mshahara wake wa Sh. milioni 2 kwa mwezi, wakati ripoti nyingine zinadai kuwa ameahidiwa Sh. milioni 30, gari na mshahara wake aliokuwa akilipwa Azam wa Sh. milioni 2 kwa mwezi.

"Ngassa ameahidiwa Sh. milioni 12 za kutia mfukoni, gari na mshahara wa kila mwezi wa Sh. milioni 2, ambapo moja itatolewa na Hanspope na moja ndio wamesaini Simba katika mkataba," kilisema chanzo hicho. 

No comments:

Post a Comment