Friday, August 3, 2012

SOMA SABABU ZILIZOTOLEWA NA JAJI KUSITISHA MGOMO WA WALIMU

Rais wa CWT, Gratian Mukoba.

Rais Jakaya Kikwete
*CWT KUTOA TAMKO KESHO, YAKUNWA NA KAULI YA RAIS KIKWETE
Jaji Sophy Wambura wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi Kanda ya Dar es Salaam ametoa pigo la aina yake kwa walimu nchini baada ya kuwaamuru kusitisha mara moja mgomo ulioitishwa chama chao (CWT) kwa maelezo kuwa ni batili na pia akawataka wawalipe fidia wanafunzi walioathiriwa na hatua yao hiyo.

Jaji Wambura ametoa hukumu hiyo leo baada ya juzi na Jumatatu kupokea hoja za walimu kupitia CWT na zile za kutaka kusitishwa kwa mgomo zilizotolewa na serikali. 

Kutokana na uamuzi wake huo, Jaji Wambura akawaamuru viongozi wa  CWT kuwatangazia walimu kwamba hakuna mgomo na hivyo warejee shuleni kuendelea na kazi.

Akitoa ufafanuzi juu ya hukumu yake, Jaji Wambura alisema kwamba mgomo huo ni batili kwa sababu CWT ilitakiwa kutoa taarifa ya saa 48 kwa Serikali kama sheria inavyoelekeza na kutoa nafasi kwa mwajiri kulinda mali zake, jambo ambalo halikutekelezwa kwani CWT ilitangaza kuanza mgomo Julai 27 huku ikijua kwamba kulikuwa na siku ya mapumziko.

Alisema kutokana na tangazo la CWT, mgomo huo ulianza Jumatatu ya Julai 30, ikiwa ni kabla ya kutimia kwa saa 48 na hivyo mwajiri ambaye ni Serikali, hakupata muda wa kulinda mali zake.

Jaji huyo akaitaja sababu ya pili iliyoufanya mgomo wa walimu uwe batili ni kitendo chao cha kutotangaza ukomo wake na pia upigaji wa kura za kuunga mkono zoezi hilo haukukamilika kwa wanachama wote wa chama hicho.

Akaiamuru CWT ilipe hasara ambayo serikali imepata kutokana na mgomo huo na vilevile kuwafidia wanafunzi wote nchini kutokana na athari walizopata katika siku nne za kufanyika kwa mgomo huo.

“Mahakama inawaamuru viongozi wa chama hicho kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwatangazia walimu kuwa hakuna mgomo na warejee kazini.”

Hata hivyo, rais wa CWT, Gratian Mukoba alishasema jana kwamba watakata rufaa ikiwa mahakama itawataka warejee kazini huku wao wakiamini kwamba wana haki ya kuendelea na mgogmo huo.

Kabla ya uamuzi wa mahakama kuu leo, CWT kupitia kwa katibu wake Oluoch imeelezea kufurahishwa kwake na kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa jana wakati akizungumza na wahariri wa habri kuwa anatambua madai yao.

“Huko nyuma tulikuwa tukipuuzwa sana na serikali. Tumefurahishwa na kauli yake ya kusema kwamba majadiliano yanaendelea kwani tangu Juni mwaka jana tulitaka tuingie kwenye majadiliano, lakini haikuwezekana,” alisema Oluoch

No comments:

Post a Comment