Luka Modric... kifaa kipya Real Madrid |
KIUNGO wa Tottenham, Luka Modric ametua katika jiji la Madrid ili kukamilisha leo hii uhamisho wake wa kujiunga na Real Madrid ambao ni mabingwa wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania.
Gazeti la Daily Mail limesema kuwa Modric atafanyiwa uchunguzi wa vipimo vya afya leo baada ya Real Madrid kukamilisha mazungumzo ya uhamisho wake akitokea Tottenham na akifuzu, atasaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo inayonolewa na kocha Jose Mourinho.
Ofa ya mwisho iliyotolewa kwa ajili ya kumnasa kiungo huyo wa kimataifa wa Croatia mwenye miaka 26, na ambayo ilikataliwa na Tottenham, ilikuwa ni paundi za England milioni 38 (Sh. bilioni 95), zikihusisha fedha taslim kiasi cha paundi za England milioni 30 (Sh. bilioni 75) huku sehemu iliyobaki ikitarajiwa kulipwa kulingana na kiwango atakachoonyesha na muda wa mkataba atakaosaini Modric.
Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy amekuwa mgumu na kusema kwamba hatakubali dau lolote la uhamisho wa Modric litakalokuwa chini ya paundi za England milioni 40 (Sh. bilioni 100) na pia hafurahishiwi na kiasi cha asilimia ya fedha kitakachotolewa na timu hiyo ikwia Modric ataonyesha kiwango cha juu na kuipa mafanikio Real Madrid ya Mourinho.
Hata hivyo, Real Madrid wamewaambia maafisa wa Tottenham kwamba sasa wako tayari kuongeza kiasi cha pesa taslim ya ada watakayolipa na kuwa paundi za England milioni 34 (Sh. bilioni 85), na hivyo wanaamini kwamba watamalizana kabla ya mwisho wa wiki hii.
Luka Modric ametua jijini Madrid baada ya kuichezea timu yake ya taifa ya Croatia iliyocheza dhidi ya Uswisi jana usiku.
Awali, Modric alikuwa na mgogoro mzito na Tottenham baada ya kutaka auzwe kwa Real Madrid mwanzoni mwa kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi.
Alichelewa kuripoti katika kambi yao ya kujiandaa na msimu mpya na pia alikataa kujiunga na wenzake waliokwenda Marekani kucheza mechi za kirafiki za maandalizi ya msimu.
Taarifa za uhamisho wa Modric kwenda Real Madrid zimekuja ikiwa ni miezi 12 tu tangu alipoomba kuondoka Tottenham ili atue Chelsea, ombi ambalo Levy alilitupilia mbali licha ya Chelsea kukubali kulipa ada ya uhamisho ya paundi za England milioni 40 (Sh. bilioni 100), ikiwa ni siku chache tu kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi, Agosti 2011.
No comments:
Post a Comment