Monday, August 13, 2012

HATIMAYE TOTTENHAM WAKUBALI LUKA MODRIC AENDE REAL MADRID KWA BIL. 60/-


Luka Modric
MADRID, Hispania
REAL Madrid wamesema kuwa tayari wameshafikia makubaliano na Tottenham kuhusiana na usajili wa kiungo wa kimataifa wa Croatia, Luka Modric ili aichezee kuanzia msimu ujao wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania.

Gazeti la AS limeripoti leo kuwa mwafaka umefikiwa baina ya klabu hizo mbili na kitu pekee kinachosubiriwa sasa ni ombi la Tottenham la kutaka wapewe muda wa kusaka kiungo mwingine mbadala kabla ya kumruhusu Modric.

Kwa mujibu wa makubaliano yao, ada ya uhamisho ya Modric itakuwa euro milioni 32 (Sh. bilioni 60) pamoja na 'bonasi' zitakazotokana na idadi ya mechi atakazocheza akiwa Real Madrid na mafanikio atakayopata.

Awali, mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy alitaka bei ya mwisho ya kumuuzia Modric kuwa euro milioni 38 (Sh. bilioni 72), lakini sasa amelainika na kukubali kupunguza kiwango hicho.

Ikiwa makubaliano hayo yatatekelezwa yataipa nafuu kubwa Real, ambayo ilishuhudia 'ofa' ya PSG ya Ufaransa kutaka kumtwaa Modric kwa euro milioni 45 (Sh. bilioni 86) ikikataliwa na mchezaji huyo aliyesisitiza kwamba hataki kwenda kokote isipokuwa kwa mabingwa hao wa La Liga, Real Madrid

No comments:

Post a Comment