Waziri wa Kazi na Ajira, Mhe. Gaudentia Kabaka |
Serikali imewaondoa hofu wafanyakazi
nchini kote kuhusiana na utata juu ya fao la kujitoa baada ya kutangaza rasmi
jioni hii kwamba inakwenda kukifutilia mbali kipengele kinachowazuia kuchukua
fao hilo.
Waziri wa Kazi na Ajira, Mhe.
Gaudentia Kabaka, ameyasema hayo bungeni jioni hii wakati akijibu swali lililotaka
kujua msimamo wa serikali juu ya agizo la hivi karibuni lililotolewa na Mamlaka
ya Mifuko ya Hifadhi (SSRA) kuwa kuanzia Julai 20, 2012, hakuna mfanyakazi
atakayeruhusiwa kuchukua fao la kujitoa kwa maelezo kwamba sheria iliyopitishwa na
Bunge April, 2012 inazuia jambo hilo.
Waziri Kabaka alitakiwa pia kutoa
kauli ya serikali kuhusiana na taarifa kwamba wafanyakazi wa migodini wamegoma
kwa sababu ya kupinga kipengele hicho cha “kinyonyaji” cha sheria ya SSRA kinachozuia
wafanyakazi kulipwa fao la kujitoa.
Akijibu swali hilo wakati bunge lilipokaa kama kamati kupitia
vifungu vya bajeti ya wizara yake jioni hii, Mhe. Kabaka akawataka wafanyakazi wa
migodini na kwingineko nchini kuwa na subira kwani sheria hiyo itafanyiwa marekebisho na kuletwa tena katika kikao kijacho cha
Bunge ili kuondoa kipengele kinacholalamikiwa.
“Nawasihi wafanyakazi wa migodini wawe
na subira na kuendelea na kazi kwa amani… ni kwa sababu kikao kijacho si mbali
sana, nadhani ni Novemba… au mwezi mmoja na nusu hivi ujao… kipengele hicho
kitafanyiwa marekebisho,” alisema Waziri Kabaka na kushangiliwa na wabunge.
Hivi karibuni, Mkurugenzi wa SSRA, Irene
Isaka alizua mtafaruku na taharuki kubwa miongoni mwa wafanyakazi nchini (hasa
vijana) baada ya kutoa tangazo la kuzuia uchukuaji wa fao la kujitoa hadi
watakapotimiza miaka 55 na 60, akidai kwamba kufanya hivyo ni kwenda kinyume na
sheria ya mifuko ya hifadhi iliyopitishwa na bunge April.
Wafanyakazi wengi, kupitia vyama vyao mbalimbali
walikuja juu na kupinga vikali sheria hiyo kwa kusema kwamba ni ya “kinyonyaji”
kwani wastani wa umri wa kuishi kwa Watanzania uko chini ya miaka 55 na pia, kazi nyingi siku hizi ni za
mikataba na hivyo wengi hawana uhakika wa kuendelea na ajira zao hadi kufikia
umri huo.
Kuona hivyo, wabunge nao wakaja juu. Mbunge wa Kisarawe, Mhe. Suleiman Jaffu, akawasilisha jana hoja ya
kutaka sheria iliyounda SSRA ipitiwe upya na kuondoa kipengele
kinachozuia wafanyakazi kuchukua ‘fao la kujitoa’.
No comments:
Post a Comment