Tuesday, August 7, 2012

MAICON AITOSA PSG ATUE KWA MOURINHO REAL MADRID


Maicon

Maicon (kulia) na aliyekuwa kocha wa Inter Milan, Jose Mourinho  wakishangilia ubingwa wa Italia msimu wa 2009/10.
MILAN, Italia
BEKI wa kulia wa Inter Milan, Maicon amekataa ‘ofa’ ya kwenda kuichezea Paris Saint-Germain ili atimize dhamira yake ya kwenda Real Madrid na kuungana tena na kocha wake wa zamani, Jose Mourinho, kwa mujibu wa taarifa za Sky Sport.

Beki huyo mwenye miaka 31, hana nafasi Inter na matokeo yake amekuwa akihusishwa na uvumi mwingi katika wiki kadhaa zilizopita, huku klabu kama PSG, Chelsea na Madrid zikitajwa kumuwania.

Wakala wa beki huyo wa kimataifa wa Brazil amethibitisha kwamba mteja wake anajihisi kuwa sasa,"Ni wakati mwafaka wa kuondoka ", na beki huyo hajajumuishwa katika kikosi cha Inter kitakachoshiriki Ligi ya Europa kwa kuanzia hatua ya mchujo dhidi ya Hajduk Split.

Taarifa zimedai kwamba kocha Carlo Ancelotti wa PSG ameandaa ofa ya kumnunua kwa euro milioni10, dau ambalo linakubaliwa kirahisi na rais wa Inter, Massimo Moratti ambaye anasaka fedha za kumnunulia yosso wa klabu ya Sao Paulo, Mbrazili Lucas Moura.

Hata hivyo, Maicon hayuko tayari kwenda kucheza katika timu hiyo ya Ligue 1, Ligi Kuu ya Ufaransa, na badala yake angependa kuhamia kwa Real ambao ni mabingwa wa La Liga, au kwa Chelsea ambao wanashikilia taji la Klabu Bingwa Ulaya.

Mkataba wa Maicon unamalizika mwishoni mwa msimu ujao na hadi sasa hakuna harakati zozote zinazofanywa na Inter kwa nia ya kumpa ofa ya kuongeza mkataba.

Maicon, aliyeichezea Monaco kwa misimu miwili kabla ya kuhamia Inter mwaka 2006, anaweza hata kuongeza mkataba, lakini taarifa zilizopo zinadai kwamba kuna uwezekano mdogo wa kufanyika kwa jambo hilo. Maicon alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Inter kilichoweka historia nchini Italia kwa kutwaa mataji yote wakati kikiongozwa na Mourinho mwaka 2009.   

Wakati huo huo, Moratti alithibitisha juzi kwamba Inter wamejiondoa katika vita ya kumuwania Lucas Moura.

No comments:

Post a Comment