Fabrice Muamba.....kwaherini wapendwa. Nimelazimika kustaafu na hamtaniona tena uwanjani...! |
Fabrice Muamba akimwaga machozi baada ya kusalimia mashabiki kwejnye Uwanja wa Wembley kabla ya mechi ya fainali ya Kombe la FA. |
Fabrice Muamba akiwajibika uwanjani kabla ya kuanguka ghafla katika mechi yao ya Kombe la FA dhidi ya Tottenham |
LONDON, England
KIUNGO Fabrice Muamba amelazimika
kustaafu soka kutokana na ushauri wa madaktari, klabu yake ya Bolton Wanderers
inayoshiriki Ligi Kuu ya England imesema katika taarifa yake leo.
Muamba, 24, alikuwa ni kama amekufa
baada ya moyo wake kusimama ghafla katika mechi yao ya Machi ya Kombe la FA dhidi ya
Tottenham Hotspur kwenye Uwanja wa White Hart Lane wakati
alipoanguka uwanjani na kuhitaji vifaa maalum vya kuokoa maisha yake.
Moyo wake ulisimama kwa dakika 78
lakini kiungo huyo wa zamani akapona kimiujiza, ikiwa ni baada ya kulazwa kwa
wiki nne katika Hospitali ya London.
Muamba alikwenda Ubelgiji wiki
iliyopita kufuata ushauri wa kitabibu kutoka kwa mtaalam bingwa wa magonjwa ya
moyo, lakini matumaini yake ya kurejea tena uwanjani ili kuendelea na soka
yalifutwa.
"Taarifa nilizopata ni wazi kwamba
sio zile nilizozitarajia, na hii
inamaanisha kwamba sasa natangaza kustaafu soka la kulipwa," amesema
Muamba kupitia tovuti ya klabu yake ya Bolton (www.bwfc.co.uk)
"Tangu nipate matatizo ya moyo na
kutolewa hospitali, nimekuwa na matumaini makubwa kwamba siku moja nitaweza
kurudi tena uwanjani na kuendelea kuichezea tena Bolton Wanderers.
"Soka nd'o maisha yangu tangu
nikiwa mvulana mdogo na mchezo huu umenipatia fursa nyingi sana."
Muamba alihamia London akitokea
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati akiwa na miaka 11 na amewahi kuzichezea
timu za ngazi zote za taifa za vijana za England kuanzia U-16 hado U-21.
Aliwahi pia kuichezea Arsenal, ambako
mchezaji mwenzake wa zamani, Robin van Persie alisema kwamba mara zote alikuwa
mwenye "sura ya kutabasamu" na pia aliwahi kuichezea Birmingham City.
"Soka limempoteza mtu mwema,"
amesema kocha wa zamani wa Birmingham, Alex McLeish.
Kocha wa Bolton, Owen Coyle pia
alizungumzia namna anavyomkubali Muamba.
"Kila mmoja ameona ni namna gani
alivyokuwa mpambanaji ngangari wa kiakili na kimwili.”
No comments:
Post a Comment