Wednesday, August 15, 2012

HATIMAYE MAHAKAMA YA RUFAA KUSIKILIZA UTATA WA UMRI WA LULU, JAJI MKUU OTHMAN CHANDE APANGA SHAURI LA MSANII HUYO LIANZE KUSIKILIZWA MWEZI UJAO

Elizabeth Michael 'Lulu' akiwa katikati ya ulinzi mzito
Jaji Mkuu Othman Chande... ndiye aliyepanga shauri la Lulu lianze kusikilizwa mwei ujao
Hapa Lulu ni kabla hajakumbana na matatizo yanayomkabili sasa mahakamani

HATIMAYE Mahakama ya Rufani imepanga kusikiliza maombi ya kuchunguza utata wa umri sahihi wa nyota wa filamu nchini, Elizabeth Michael 'Lulu' (18), ambaye anadai kuwa kuwa na umri wa miaka 17 tofauti na ilivyo katika hati ya mashtaka dhidi ya tuhuma zinazomkabili za mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba (28).

Jaji Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande, amepanga shauri hilo lianze kusikilizwa Septemba lakini bado halijapangiwa jaji wala tarehe.


Upande wa Jamhuri, awali, uliwasilisha maombi katika Mahakama ya Rufani wakiitaka ifanye mapitio ya uamuzi uliotolewa na Jaji Dk. Fauz Twaib aliyekubali kusikiliza maombi hayo katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.


Hata hivyo, upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Keneddy Fungamtama, Fullujens Massawe na Peter Kibatala, uliwasilisha hati ya dharura kuiomba mahakama hiyo kusikiliza maombi hayo haraka na kuyatolea uamuzi.


Awali, mahakama kuu iliziamuru pande zote mbili kuwasilisha vielelezo dhidi ya maombi hayo ambapo baada ya hatua hiyo, ndipo upande wa Jamhuri ulipopeleka maombi Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Jaji Dk. Twaib.


Katika maombi hayo, mshtakiwa anadai kuwa umri wake ni miaka 17 na sio miaka 18 kama ilivyoandikwa kwenye hati ya mashtaka na ameomba mahakama kuu kuchunguza utata huo na kutolea uamuzi maombi yake.


Upande wa Jamhuri unawakilishwa na mawakili wa serikali, Shadrack Kimaro akisaidiana na Elizabeth Kaganda.


Katika kesi ya msingi, Lulu anadaiwa kuwa Aprili 7 mwaka huu, akiwa katika eneo la Sinza Vatican jijini Dar es Salaam, alimuua Steven Kanumba.

No comments:

Post a Comment