Straika Emmanuel Okwi |
BERNE,
Uswisi
KLABU ya
Salzburg ya Austria ambayo mchezaji wa Simba, Mganda Emmanuel Okwi amedaiwa
kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa imeanza vibaya kampeni zake
za kuwania taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya kupata kipigo cha
ugenini cha bao 1-0 kutoka kwa FC Dudelange ya Luxemburg katika mechi yao ya
hatua ya mchujo ya michuano hiyo jana.
Salzburg
ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Austria (Bundesliga), hawajawahi kufikia hatua
ya makundi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya tangu walipotwaliwa na Red Bulls mwaka
2005, licha ya wamiliki hao wapya kumwaga fedha nyingi za kuiendeshea timu
hiyo.
Aurelien
Joachim alifunga bao pekee lililowaliza Salzburg baada ya kupiga shuti kali
kutoka umbali wa mita 25 zikiwa zimebaki dakika 15 kabla ya kumalizika kwa muda
wa kawaida. Mtokea benchi Jonathan Soriano wa Salzburg alitolewa nje kwa kadi
ya pili ya njano katika dakika ya 90.
Hivi
karibuni, Okwi alidaiwa kwenda Salzburg ambako atafanyiwa majaribio ya
kuichezea klabu hiyo. Taarifa zaidi kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa klabu yake
ya Simba, Godfrey Nyange ‘Kaburu’, zilieleza kuwa akishindwa kuishawishi
Salzburg, Okwi atakwenda kujaribiwa na timu za Italia.
Imedaiwa
vilevile kuwa Okwi ambaye pia ni mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda,
amezivutia klabu za Orlando Pirates na Mamelodi Sundows zinazoshiriki Ligi Kuu
ya Afrika Kusini.
Mbali na
Salzburg ya Okwi, matokeo ya baadhi ya mechi zilizochezwa juzi za hatua ya
mchujo ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ni pamoja na ushindi wa 4-1 walioupata
mabingwa wa Serbia, Partizan Belgrade dhidi ya FC Valletta na Liberec ya
Czech ikashinda nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya Shakhtar Donetsk ya Ukraine.
No comments:
Post a Comment