![]() |
Fredrick Mwakalebela |
![]() |
Mkurugenzi wa Takukuru, Dk. Edward Hosea |
Aliyekuwa Katibu Mkuu
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela anasakwa kwa udi na
uvumba na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) ili
afikishwe mahakamani kukabiliana na kesi inayomkabili ya kudaiwa kutoa rushwa
wakati akiwania kupitishwa kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi
ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2010.
Notisi iliyotolewa
jana na Takukuru inamtaka Mwakalebela kutii wito wa kujisamilisha mwenyewe
katika ofisi za Takukuru kabla hajakamatwa kwa mujibu wa hati ya mashitaka
iliyoandaliwa.
Taasisi hiyo imefikia
uamuzi huo baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa kutupilia mbali
hoja mbili za kesi ya rufani dhidi ya Jamhuri, namba 13 ya mwaka 2010 iliyokuwa
ikiiomba mahakama kuu kutolea uamuzi mapingamizi ya kisheria ambayo mahakama ya
hakimu mkazi mkoa wa Iringa ilishindwa kuyatolea uamuzi na mengine kufanyiwa
maamuzi kimakosa.
Stephen Mafipa ambaye
ni Kaimu Kamanda wa Takukuru mkoa wa Iringa, amesema taasisi hiyo hivi sasa
inamtafuta Mwakalebela popote pale alipo ili imfikishe upya mahakamani kujibu
tuhuma zinazomkabili baada ya mahakama kuu kutupilia mbali rufaa hiyo.
Mwakalebela,
aliyekuwa kinara wa kinyang’anyiro cha uchaguzi ndani ya CCM kabla ya
kuenguliwa, alikata rufaa katika Mahakama kuu ya Tanzania, akipinga hati ya
mashitaka iliyoandaliwa na jamhuri dhidi yake, akidai kwamba haitengenezi kosa
la jinai kisheria kwa kuwa makosa yote yalivyotajwa.
Katibu huyo wa zamani
wa TFF alihoji vilevile uhalali wa kifungu cha 21 (1) (a) na kifungu cha 24 (8)
cha Sheria ya uchaguzi namba 6 ya mwaka 2010 ambacho ameshitakiwa nacho,akidai kwamba
hicho pia hakitengenezi kosa la jinai kisheria.
Katika kesi ya
msingi, Mwakalebela anadaiwa alitenda kosa hilo Juni mwaka 2010 katika Kijiji
cha Mkoga, Manispaa ya Iringa ambapo anadaiwa kutoa hongo ya Sh.100,000 kwa
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Hamisi Luhanga ili azigawe kwa wapiga kura 30 wa
CCM ili wampigie kura za maoni za kumchagua Agosti mwaka huo kuwa mgombea
ubunge wa chama hicho.
Awali, akisoma hukumu
hiyo ya kutupilia mbali hoja hizo, Jaji Rehema Mkuye alisema amezipitia hoja za
pande zote mbili na kuona hoja ya kwanza ingekuwa na nguvu kisheria kama
mashahidi wangekuwa wameitwa na kisha kutoa ushahidi wao.
No comments:
Post a Comment