![]() |
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah |
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), Angetile Osiah, amewataka viongozi wa Simba na klabu nyingine
nchini kuacha tabia ya kujisafisha kwa wanachama wao kwa kutupia mzigo wa
lawama shirikisho hilo pindi wanapoteleza kwa kufanya mambo kinyume cha
utaratibu.
Akizungumza leo katika mahojiano yake
na kituo kimoja cha luninga kuhusiana na utata wa beki Kevin Yondani
aliyeikacha Simba na kuichezea Yanga katika michuano inayoendelea ya Ligi ya
Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), katibu huyo alisema kuwa kuna makosa
yamefanywa na uongozi wa Simba kuhusiana na mkataba wa mchezaji huyo; na kwamba
sasa wanachofanya ni kuwatupia mzigo TFF.
“Siasa za kutupia mzigo TFF zimepitwa
na wakati,” alisema Angetile na kutaka viongozi wa klabu waache tabia hiyo.
Akifafanua, Angetile alisema kuwa
mkataba wa awali wa Yondani na klabu ya Simba ulimalizika Mei 31, 2012, na kwa
mujibu wa kanuni, mkataba mwingine wa kumuongezea Yondani ulipaswa kuonyesha
kuwa unaanzia katika kipindi cha kabla ya kumalizika kwa mkataba wa awali, akitolea
mfano Mei 29.
Hata hivyo, akasema kuwa mkataba
mwingine unaolalamikiwa na Simba kuwa ndio uliomuongezea Yondani kipindi cha
kubaki klabuni kwao unaonyesha kuwa unaanzia Juni 1, 2012, jambo ambalo si
sahihi kwani tarehe hiyo inaashiria kuwa huo sasa ni mkataba mpya.
Katibu huyo aliongeza kuwa kasoro
nyingine za mkataba unaolalamikiwa na viongozi wa Simba ni pamoja na tarehe ya
kusainiwa kwake, ambapo unaonyesha kuwa uliingiwa Desemba 23, 2012.
“Hili nalo ni tatizo kwa sababu siku
hiyo bado haijafikiwa,” alisema Angetile.
Akaongeza kuwa kwa sababu hiyo, wao
(TFF) hawawezi kumzuia Yondani kuichezea Yanga katika michuano ya Kagame kwa
mkataba wa Simba ambao ni “controversial” (wenye utata).
Akijibu tuhuma kwamba kuna maamuzi
yaliyofanywa kwa kutegemea uamuzi wake binafsi, Angetile alisema kuwa hilo
kamwe haliwezekani kwani TFF ni taasisi.
“Hii (TFF) ni taasisi. Mtu huwezi
kufanya maamuzi peke yako,” alisema, kabla ya kueleza zaidi kuwa suala la
kuongeza mkataba wa wachezaji (kama Yondani) liko katika mamlaka ya katibu na
hivyo hawakuwa tayari kutumia “controversial documents” (nyaraka zenye utata)
kumzuia Yondani asicheze Kagame.
Angetile alisisitiza kuwa kuwa enzi za
kufungia wachezaji zimeshapita kwani hivi sasa jukumu la kusajili liko kwa
klabu zenyewe.
SOMO LA FIGO KUTOKA BARCA KWENDA REAL
Katika hatua nyingine, Angetile alizitaka
klabu za soka nchini kusajili kwa kuzingatia vigezo vya kitaalam na kuweka
kando ushabiki na siasa, huku pia akizishauri kubadilika na kuiacha kugombania
wachezaji.
Akashauri kwamba badala ya kutumia
muda mwingi kulumbana, klabu zikae na kuzungumza juu ya kuuziana wachezaji
wanaoonyesha dhamira ya kutaka kuhamia timu nyingine.
Katibu huyo alihoji kuwa, kama iliwezekana
kwa straika Luis Figo kuihama Barcelona na kwenda kwa mahasimu wao wa jadi Real
Madrid, kwanini ishindikane kwa wachezaji wa klabu za hapa nchini kuuziana
wachezaji bila kuzozana?
“Cha muhimu ni klabu yenye mchezaji
kutaja bei yao,” alisema Angetile.
No comments:
Post a Comment