Wachezaji wa Yanga wakishangilia baada ya kuifunga APR leo jioni. |
Godfrey Taita (kushoto) wa Yanga akiukosa mpira mbele ya wachezaji wa APR kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo jioni. |
Ni raha tuuu.... Mashabiki wa Yanga wakisherehekea kutinga fainali baada ya kuilaza APR kwenye Uwanja wa Taifa leo jioni |
Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet (kushoto) akizungumza na kocha wa APR, Arnie Brandts, wakati wa mechi ya timu zao leo jioni. |
Winga Kipre Tchetche (kulia) akizuiwa na beki wa AS Vita wakati wa mechi yao iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa leo saa 8:00 mchana. Azam walishinda 2-1. |
Na Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga, watacheza fainali itakayokutanisha timu za Tanzania tupu dhidi ya Azam Jumamosi baada ya timu hizo kushinda mechi zao za nusu fainali kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.
Azam, ambao wanashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza, walitangulia fainali baada ya kuifunga AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza ya nusu fainali iliyochezwa uwanjani hapo mapema leo mchana.
John Bocco alifunga bao lake la tano katika michuano hiyo kwa kichwa katika dakika ya 67, akisawazisha bao walilotanguliwa mapema dakika ya 35 kupitia kwa Alfred Mfongang, lakini winga aliyeingia kutokea benchi Mrisho Ngassa alifunga la ushindi katika dakika ya 88.
Mshambuliaji Hamis Kiiza 'Diego' aliifungia Yanga bao pekee la ushindi katika dakika ya 100 kufuatia krosi ya kiungo Haruna Niyonzima na kuwapeleka Yanga katika fainali ya pili mfululizo baada ya kurejeshwa katika michuano hiyo kufuatia kusamehemewa adhabu yao ya kifungo cha miaka mitatu wakiwa tayari wametumikia miaka miwili.
Hata hivyo, Yanga ambao katika kipindi cha pili walitawala mchezo hadi kwa asilimia 63 dhidi ya 37 za APR, walilalazimika kupambana kiume ili kujilinda baada ya kubaki 10 uwanjani kufuatia kutolewa kwa kadi ya pili ya njano kwa beki wao wa kulia, Godfrey Taita, kwa kuchelewesha mpira wakati tayari wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Ngassa, ambaye anaonekana kukosa furaha katika kikosi hicho cha Azam kutokana na kusota benchi kufuatia nafasi yake uwanjani kuchukuliwa na winga mwenye nguvu wa Ivory Coast, Kipre Tchetche, alichochea tena uvumi kwamba anataka kurejea Yanga kufuatia kuvaa na kisha kuibusu jezi ya klabu yake ya zamani ya Yanga.
Hata hivyo, Kocha wa Azam, Muingereza Stewart Hall alipoulizwa na mtangazaji Thomas Mlambo wa kituo cha televisheni cha Supersport cha Afrika Kusini sababu za kutomuanzisha Ngassa, alisema: “Najua ni mchezaji mzuri, ninamuhitaji, lakini nataka ajitume zaidi.”
Kocha wa APR, Ernie Brandts, ambaye alishuhudia timu yake ikifungwa mechi ya pili na Yanga ndani ya wiki moja baada ya kulala 2-0 katika mechi yao ya mwisho ya Kundi C Ijumaa iliyopita, alimlalamikia mwamuzi wa mechi hiyo akisema: “Hii ni Afrika. Mchezaji analala uwanjani kwa dakika sita lakini mwisho wa mechi zinaongezwa dakika tatu.”
Brandts alionekana kukerwa na mbinu za kupoteza muda za kipa wa Yanga, Ali Mustapha ‘Barthez’, aliyekuwa akilala chini mara kwa mara wakati wakiwa 10 uwanjani huku mechi ikielekea ukingoni.
“Goli limepatikana baada refa kuruhusu mechi iendelee wakati kulikuwa na faulo. Hii ni Afrika. Hii ni Afrika,” alilalamika Brandts.
Kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet, hata hivyo, alimshangaa Brandts kudai timu yake ilionewa ilhali refa alifanya makosa kwa pande zote.
"Kama anadai kwamba kulikuwa na faulo kabla ya Yanga kurusha haraka mpira na kufunga goli, basi wachezaji wawili wa APR walipaswa kutolewa kwa kadi nyekundu katika tukio hilo.
"Mchezaji wangu katolewa kwa kadi nyekundu nyepesi wakati wachezaji wa APR wamecheza rafu nyingi, wamemuimiza beki wangu wa kulia (Juma Abdul aliyetoka dakika ya 27) na hawakufanywa kitu. Kama makosa refa alifanya na aliyafanya kwa pande zote.
“Kipindi cha kwanza hatukucheza vizuri, lakini tulirejea vyema katika kipindi cha pili tukatawala mechi na hata katika dakika 30 za nyingeza, ni vizuri kumpongeza mshindi,” alisema Saintfiet, ambaye anaiongoza Yanga katika mechi zake za kwanza za kimashindano tangu akabidhiwe mikoba hivi karibuni kutoka kwa kocha Mserbia Kostadin Papic aliyemaliza mkataba wake.
Kikosi cha Yanga kilikuwa: Ali Mustapha 'Barthez', Juma Abdul/ Shamte Ali (dk.27)/ Rashid Gumbo (dk.86), Godfrey Taita, David Luhende, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Oscar Joshua, Athuman Idd 'Chuji', Stephano Mwasika, Haruna Niyonzima, Said Bahanuz na Hamis Kiiza 'Diego'.
Kikosi cha Azam kilikuwa: Deogratias Munishi, Ibrahim Shikala, Erasto Nyoni, Said Moradi, Aggrey Morris, Jabir Aziz, Kipre Tchetche/Mrisho Ngassa, Salum Abubakar, John Bocco 'Adebayor', Ibrahim Mwaipopo na Ramadhani Chombo 'Redondo'.
No comments:
Post a Comment