![]() |
Wachezaji wa Ureno wakiwa viroho juu wakati wa hatua ya 'matuta' dhidi ya Hispania katika nusu fainali ya Euro 2012. Nani yuko kushoto, Ronaldo kulia. |
![]() |
Nani (kushoto) na Ronaldo wa Ureno wakishangilia katika mechi mojawapo ya fainali za Euro 2012 |
PORTO, Ureno
WINGA Luis
Nani wa timu ya taifa ya Ureno amefichua kwa mara nyingine kwamba nahodha wake Cristiano
Ronaldo aling’ang’ania kupiga penati ya mwisho wakati wa hatua ya ‘matuta’ ya
mechi yao ya nusu fainali ya Euro 2012 dhidi ya Hispania.
Kutokana na
kukosa kwa Joao Moutinho na Bruno Alves, nyota huyo wa Real Madrid alikoseshwa
nafasi ya kupiga penati yake, ambayo pengine ingewavusha kwa hatua ya fainali
baada ya goli alilofunga Cesc Fabregas kuwahakikishia Hispania ushindi wa
penati 4-2.
Nani ambaye
pia ni winga wa Manchester United, amesema kwamba hakukuwa na utata wowote
kuhusiana na uchaguzi wa watu wa kutangulia kupiga penati, lakini aliongeza
kwamba Ronaldo alitaka apige penati ya tano.
“Sidhani
kama kulikuwa na tatizo au makosa yoyote yaliyofanyika,” winga huyo mwenye miaka
25 aliliambia gazeti la Times of India.
“Cristiano alitaka
kupiga penati ya mwisho. Nilimwambia kocha niko tayari kupiga penati yoyote ile.
Kwangu sikuona kama kuna tatizo kwa sababu mikwaju ya penati huwa inategemea
bahati na kwakweli hatukustahili kutolewa kivile.”
Licha ya
kuondolewa katika nusu fainali hiyo, Nani anaamini kwamba kikosi chao
kilichoongozwa na kocha Paulo Bento kinastahili kujivunia kiwango
walichoonyesha katika fainali za Euro 2012 zilizofanyika katika nchi za Poland na
Ukraine.
“Ni wazi
kwamba tuliondoka tukiwa na huzuni tele baada ya kutolewa kwa sababu tulikaribia
kufika fainali, hata hivyo tunaweza kujifariji kutokana na kile tulichokifanya.
“Tulijitolea
kadri ya uwezo wetu wote. Tulionyesha kiwango cha juu. Mwishowe Hispania
walikuwa na bahati zaidi kulinganisha na sisi kwa sababu kila zinapopigwa
penati, bahati ndio huamua mshindi.
“Wao ni mabingwa
waliostahili, lakini nadhani kwamba katika nusu fainali yetu tulistahili kuwafunga.
Kwahiyo watu wa Ureno wanaweza kujivunia timu yao. Tuna huzuni kwa sababu
tulistahili kutinga fainali, hata hivyo tulirudi nyumbani huku vichwa vyetu vikiwa juu,” alihitimisha.
Hispania ambao
pia ni mabingwa wa Dunia, waliendeleza moto wao kwa kuwashindilia Italia mabao 4-0
katika mechi yao ya fainali na kuatwaa ubingwa wa tatu mfululizo katika
michuano ya kimataifa.
No comments:
Post a Comment