Wednesday, July 11, 2012

MWANZA WATINGA NUSU FAINALI COPA COCA COLA, KINONDONI WAMWAGA VILIO

Tumaini Agustino wa Mwanza akimiliki mpira dhidi ya Yahaya Mohammed wa Kinondoni wakati wa mechi yao ya robo fainali ya michuano ya Copa Coca Cola kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam jana. Mwanza imeshinda kwa penalti 3-1 baada ya dakika 90 kumalizika kwa matokeo ya 0-0. Picha: Sanula Athanas

Ah! Vijana wananipa raha hawa....! Kocha wa timu ya taifa ya vijana, Jacob Michelsen (mwenye begi miguuni) akishuhudia mechi ya robo fainali ya Copa Coca Cola baina ya timu ya Mwanza na Kinondoni pamoja na msaidizi wake Jamhuri Kihwelu 'Julio' (wa pili kushoto) leo. Picha: Sanula Athanas 

Yohana Nicholas wa Mwanza akitoka nje ya uwanja baada ya kulimwa kadi nyekundu katika dakika ya 33 kufuatia kumchezea rafu mbaya Yahaya Mohammed wa Kinondoni leo. Picha: Sanula Athanas  
Kipa wa Mwanza, Samwel Samwel akipangua penalti ya Kinondoni. Picha: Sanula Athanas

Mfungaji wa penalti pekee ya Kinondoni, Shaban Nyenje (kushoto) akimtungua kipa wa Mwanza, Samwel Samwel wakati wa mechi yao ya robo fainali leo. Picha: Sanula Athanas

Wachezaji wa akiba wa Kinondoni wakishuhudia kutokea benchi. Picha: Sanula Athanas
Dada wa mchezaji mchezaji wa Kinondoni, Jumanne Goa (mwenye baibui) akilia huku akimbembeleza mdogo wake baada ya kufungwa kwa penalti 3-1 dhidi ya Mwanza leo. Picha: Sanula Athanas

Dada wa mchezaji mchezaji wa Kinondoni, Jumanne Goa akilia baada ya timu ya mdogo wake kufungwa kwa penalti 3-1 dhidi ya Mwanza leo. Picha: Sanula Athanas

Dada wa mchezaji mchezaji wa Kinondoni, Jumanne Goa akilia baada ya timu ya mdogo wake kufungwa kwa penalti 3-1 dhidi ya Mwanza leo. Picha: Sanula Athanas

Wachezaji wa timu ya Mwanza wakishangilia ndani mwa basi lao tayari kwa kuondoka kwenye Uwanja wa Karume baada ya kuitoa Kinondoni na kutinga nusu fainali ya Copa Coca Cola leo. Picha: Sanula Athanas 

Wachezaji wa timu ya Mwanza wakishangilia baada ya kuitoa Kinondoni na kutinga nusu fainali ya Copa Coca Cola leo. Picha: Sanula Athanas 

Wachezaji wa timu ya Mwanza wakishangilia baada ya Kinondoni kukosa penalti ya nne na kuwapa tiketi ya kutinga nusu fainali ya Copa Coca Cola leo. Picha: Sanula Athanas 


Na Sanula Athanas
TIMU ya soka ya Mwanza imetinga nusu fainali ya michuano ya vijana ya Copa Cocacola kwa ushindi wa penalti 3-1 dhidi ya Kinondoni baada ya dakika 90 kumalizika kwa matokeo ya 0-0 kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam leo.

Kipa wa Mwanza, Samwel Samwel, aliibuka shujaa wa timu yake baada ya kupangua penalti 3 kati ya 4 za hatua ya kupigiana "matuta". Penalti 3 za Mwanza zilitinga wavuni na kuhitimisha safari ya Kinondoni katika mashindano hayo.

Penalti tatu za vijana wa Mwanza wanaonolewa na kocha Daddy Gilbert, zilizopigwa na Christopher Maghingwa, Juma Masunga na Steven Lubela zilimshinda kipa Mohamed Soud. Mwanza sasa wataikabili Temeke katika nusu fainali.

Shaban Nyenje ndiye mchezaji pekee aliyefunga penalti yake kwa upande wa Kinondoni huku wachezaji wenzake Miza Abdallah, John Komba na Mbarouk Liyayala wakikosa penalti zao.

Baada ya mechi hiyo kocha Gilbert alitamba kunyakua ubingwa wa mashindano hayo mwaka huu.

"Mechi ya leo ilikuwa ngumu sana, hasa pale tulipolazimika kucheza tukiwa pungufu… vijana wanajua kwamba Mwanza na Kanda ya Ziwa yote inawategemea wapeleke kombe Mwanza, naamini tutafanya vizuri zaidi kwenye mechi inayofuata na tutatwaa ubingwa,” alisema Gilbert.

Naye shujaa wa Mwanza kwenye mechi hiyo, kipa Samwel alisema utaratibu uliotumiwa na kocha wao kwenye mechi za kirafiki kabla ya kuanza kwa mashindano hayo ndio siri ya ushindi huo.

“Nilikuwa nikijiuliza maswali mengi kuhusu utaratibu wa kocha wetu kutuchezesha tukiwa pungufu katika mechi za kirafiki kabla hatujaja kushiriki mashindano haya, leo ndio nimepata jibu, tumewamudu Kinondoni licha ya kucheza tukiwa kumi,” alisema Samwel.

Mwanza walilazimika kucheza pungufu baada ya mwamuzi Liston Hiyari kumwonesha kadi nyekundu beki Yohana Nicolaus baada ya kumchezea rafu mbaya winga wa kushoto wa Kinondoni, Yahaya Mohamed.

Mechi hiyo namba 95 ya robo fainali za michuano ya Copa Coca Cola mwaka huu kati ya Kinondoni na Mwanza ilishuhudiwa pia na wasaka vipaji kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakiongozwa na makocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 (Ngorongoro Heroes), Jacob Michelsen na Jamhuri Kiwelu ‘Julio’.

No comments:

Post a Comment