Mhe. Mwigulu (kushoto) akiteta jambo na Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai |
Mhe. Mnyika |
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) atapelekwa mbele ya
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge baada ya kushindwa kuthibitisha tuhuma
alizotoa bungeni kuwa Mbunge wa Iramba Magharibi, Mhe. Mwigulu Mchemba (CCM) ni
miongoni mwa watu waliohusika na wizi wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni
ya Nje (EPA).
Akizungumza bungeni leo, Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Job
Ndugai, alisema kuwa Mnyika aliyekuwa amepewa siku 7 za kuwasilisha ushahidi utakaothibitisha
tuhuma za wizi alizotoa dhidi ya Mwigulu, ameshindwa kufanya hivyo.
Kwa sababu hiyo, Mhe. Ndugai akasema kuwa mwongozo wake
kuhusiana na suala hilo ni kwamba, atampeleka Mnyika mbele ya Kamati ya Bunge
ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili ichukue hatua zinazostahili kwa
mujibu wa kanuni za Bunge.
Awali, kabla ya kuendelea kwa majadiliano ya makadirio na
mapato ya matumizi ya Wizara ya Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Mhe.
Mwigulu alisimama na kuomba mwongozo wa Spika kuhusiana na madai aliyotoa Mhe.
Mnyika dhidi yake ndani ya Bunge hilo kuwa yeye (Mwigulu) ni miongoni mwa watu
walioiba fedha za EPA (Sh. Bilioni 133) na akatakiwa kuthibitisha kauli yake ndani ya siku saba lakini hadi leo hajatekeleza
jambo hilo ingawa tayari siku alizopewa zimeshapita.
ILIVYOKUWA JULAI 3
Mnyika alipewa siku
saba kuanzia siku aliyotoa kauli hiyo (Julai 3) kuthibitisha tuhuma za wizi wa
fedha za EPA alizotoa dhidi ya Mhe. Mwigulu wakati wa kuchangia bajeti ya
Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora). Mwenyekiti wa Bunge, Mhe.
Jenista Mhagama, ndiye aliyempa agizo hilo baada ya kuibuka majibizano makali
wakati Mwigulu akichangia hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara
hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.
Awali, Mnyika aliomba mwongozo wa Spika na kupinga baadhi ya
maelezo ya Mwigulu ambaye katika mchango wake, aliponda baadhi ya taarifa
zilizomo kwenye hotuba ya Waziri Kivuli wa Kambi Rasmi ya Upinzani, ikiwemo
iliyodai kuwa hali ngumu ya watumishi wa serikali imewafanya walimu wa shule za
msingi kujikuta wakijihusisha na biashara huku wahadhiri wa vyuo mbalimbali vya
umma wakilazimika kufundisha pia katika vyuo vingine binafsi hadi vitatu.
Wakati mabishano hayo,
yakiendelea na wakati fulani kuwahusisha wabunge wengine kama Mchungaji
Msigwa wa Jimbo la Iringa Mjini (CHADEMA) na Mhe. George Simbachawene wa
Kibakwe(CCM), ndipo Mnyika alipomtuhumu Mwigulu kuwa naye ni miongoni mwa
watuhumiwa wa kashfa ya fedha za EPA (Sh. bilioni 133) kwani alikuwa ni
miongoni mwa watumishi wa Benki Kuu ya Tanzania ambako ndiko wizi huo ulikotokea.
Alisema kwamba inasikitisha kuona kuwa hotuba ya bajeti ya
Ofisi ya Rais (Utawala Bora) haionyeshi ni kwa jinsi gani Idara ya Usalama wa
Taifa imekuwa ikizuia uhalifu kama wa EPA.
Hata hivyo, Mwigulu
aliposimama tena siku hiyo, alianza kwa kusema kuwa wakati wizi wa EPA ukitokea
(mwaka 2005), yeye alikuwa bado ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
na kwamba, (wakati huo) hata mlango wa
kuingilia Benki Kuu alikuwa haujui.
Alisema kuwa alianza kazi BoT Oktoba, 2006.
No comments:
Post a Comment