Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai |
Mbunge wa Kigamboni kwa tiketi ya CCM, Mhe. Dk. Faustine
Ndungulile amejikuta akitimuliwa bungeni mjini Dodoma jioni hii na kutolewa na
askari hadi nje ya ukumbi baada ya kushindwa kuwasilisha ushahidi wa madai aliyotoa
awali kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (Prof. Anna
Tibaijuka) alitumia fedha za serikali kuwapeleka bungeni hapo baadhi ya
wananchi wa Kigamboni ikiwa ni sehemu ya jitihada za kusaka uungwaji mkono wa mradi
wa mji wa Kigamboni.
Aliyetoa amri ya kutimuliwa kwa Mhe. Ndungulile ni Naibu
Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai; ambaye alisema kwamba kitendo alichofanya
mbunge huyo hakikubaliki kwani ni kinyume cha kanuni za Bunge.
Mhe. Ndungulile alitoa tuhuma hizo jana wakati akichangia
makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi.
Baada ya hapo, Mhe. Ndugulile akaamriwa kuwasilisha ushahidi
wa madai yake leo jioni na aliposhindwa kufanya hivyo, ndipo Mhe. Ndugai alipomtimua
nje ya ukumbi na pia kumsimamisha kwa kumuamuru kuwa asihudhurie katika vikao
vitatu vijavyo vya Bunge kutokana na kosa hilo la kusema uongo bungeni
Mara baada ya Mhe. Ndugai kutoa hukumu hiyo, Ndungulile
alionekana kutii amri kwa kutoka nje ya ukumbi huku akisindikizwa na askari
walioamrishwa kufanya hivyo na kiti cha spika.
No comments:
Post a Comment