Mhe. Halima Mdee (aliyeinua mkono) akiwa bungeni. |
Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai amempa onyo kali Mbunge
wa Kawe kwa tiketi ya Chadema, Mhe. Halima Mdee kutokana na kile alichodai kuwa
ni tabia yake ya kutoheshimu kiti cha spika.
Mhe. Ndugai alichukua hatua hiyo baada ya kukerwa na kitendo
cha Mhe. Halima kutaka kutoa taarifa wakati yeye akiendelea kutoa mwongozo wake
dhidi ya tuhuma za Mbunge wa Kigamboni, Mhe. Dk. Faustine Ndungulile, aliyekuwa
akisomewa hukumu yake kutokana na kosa la kutoa tuhuma zisizokuwa na ushahidi dhidi
ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka.
Ndugai alisema kuwa Mhe. Halima amekuwa na tabia ya
kutoheshimu kiti cha Spika kwa kuzungumza bila kupata idhini na kwamba,
anachukua fursa hiyo kumpa onyo la mwisho kwani ni kinyume cha taratibu za
mabunge yote.
Wakati Mhe. Ndugai akiendelea kutoa maelezo yake, Mhe. Halima
alionekana akifanya jitihada za kupata nafasi ya kutoa hoja yake kwa kutamka neno
“taarifa”. Jambo hilo likamkera zaidi Mhe. Ndugai ambaye sasa alionekana kuongea
kwa ukali na kumuamuru akae chini.
Baada ya hapo, Mhe. Ndugai akazidi kumshutumu Mhe. Halima na
kusema kwamba wananchi wa Kawe wanajionea mbunge wao, akisema ni “kituko tu”.
Akamwambia zaidi kwamba anajua kuwa (Mhe. Halima) anataka umaarufu
tu kwa kutolewa nje ya ukumbi (kama ilivyokuwa kwa Ndungulile) ili kesho yake
magazeti yote yamuandike.
Kwa kutambua hilo, Ndugai akadai kuwa yeye (Mhe. Halima)
hamtoi nje na badala yake anampuuza tu.
Hayo yote yametokea jioni hii Bungeni Dodoma wakati wa kuhitimisha
mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi.
No comments:
Post a Comment