Dk. Slaa (kulia) akiwa jukwaani na mchumba wake Josephine Mushumbuzi |
Dk. Slaa akiwa na Rose Kamili |
Ile ndoa kati ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa na
mchumba wake Josephine Mushumbuzi iliyopangwa kufanyika Jumamosi ijayo (Julai
21) sasa iko njia panda baada ya Jaji Lawrance Kaduli wa Mahakama Kuu Kanda ya
Dar es Salaam anayesikiliza pingamizi la ndoa hiyo lililowekwa na aliyekuwa mke
wa Dk. Slaa, Rose Kamili kuamuru kuwa suala hilo lifikishwe tena kortini Agosti
14, ikiwa ni baada ya kupita kwa tarehe iliyopangwa
kwa ajili ya kufungwa kwa ndoa hiyo.
Mahakama hiyo imepanga kuwa Agosti 14 mwaka huu isikilize
kesi hiyo ya kusimamisha ndoa ya Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk. Willibroad Slaa na mchumba wake Josephine Mushumbuzi
inayotarajiwa kufungwa katika wilaya ya Karatu mkoani Manyara.
Jaji Kaduli, leo ameitaja kesi hiyo namba 4 ya mwaka 2012,
iliyofunguliwa na mke wa Dk, Slaa, Rose
Kamili ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema). Jaji huyo aliwataka Dk
Slaa na Josephine wajibu pingamizi hilo
la ndoa yao kwa njia ya maandishi kabla ya Julai 30, mwaka huu.
Pia alimtaka Rose Kamili kupitia wakili wake, Joseph Thadayo
kama watakuwa na majibu yoyote wayafaili Agosti 7, mwaka huu na kwamba baada ya
taratibu hizo kufanyika, Agosti 14 mwaka huu ataisikiliza kesi hiyo.
Kwa maana hiyo, ndoa hiyo iliyotajiwa kufungwa Jumamosi ijayo
ya Julai 21, haitafungwa hadi hapo Mahakama Kuu itakapotoa maamuzi juu ya
maombi hayo.
Katika kesi hiyo dhidi ya Dk Slaa na mchumba wake Josephine Mushumbusi, mlalamikaji
Rose Kamili anaiomba Mahakama kusimamisha ndoa hiyo iliyopangwa kufungwa wilayani
Karatu mkoa wa Manyara.
Rose pia anaiomba mahakama imuamuru Dk. Slaa kumlipa Sh. milioni
50 kama fidia aliyotumia kujihudumia pasipo matunzo ya mumewe huyo.
Mbunge huyo kupitia wakili wake Thadayo, anaiomba pia mahakama
iamuru Mushumbuzi amlipe Sh. milioni 500 kama fidia ya maumivu aliyoyapata
kutokana na kitendo chake cha kuingilia ndoa yao.
Katika hati hiyo ya madai, mbunge huyo anadai kuwa ndoa
inayotarajiwa kufungwa kati ya Dk.Slaa na Mushumbuzi ni batili kwa sababu kuna
ndoa nyingine halali na inayoendelea kuishi kati ya Dk. Slaa na yeye (Rose Kamili)
iliyofungwa mwaka 1985.
Alidai baada ya kufugwa kwa ndoa hiyo, Juni 18 mwaka 1987
walifanikiwa kupata mtoto wa kike anayeitwa Emiliana na baadaye Septemba 23
mwaka 1988, walipata mtoto mwingine wa kiume aitwaye Linus Amsi.
Katika uhusiano wao, Dk. Slaa akiwa ni Padri wa Kanisa la
Roman Katoliki, alifanya taratibu zilizomwondosha katika nafasi hiyo ya upadre
na kuanza maisha ya familia.
Baada ya taratibu hizo, jamii ya Watanzania iliwatambua kama
mume na mke ambapo hata kumbukumbu za hati za kimataifa kama za kusafiria
ziliwatambua wao kuwa ni wanandoa.
Rose Kamili aliendelea kudai katika maelezo hayo kuwa yeye na
Dk. Slaa waliishi maisha ya ndoa yenye amani, yaliyowawezesha kupata mali
kadhaa walizomiliki kwa pamoja ikiwemo nyumba iliyopo kwenye kiwanja namba 609
kitalu E, nyumba ya makazi iliyopo kijiji cha Gongali huko Karatu na vifaa
mbalimbali vya nyumbani.
Hati ya mashtaka imeendelea kueleza kuwa, uhusiano kati ya
Slaa na mkewe Kamili, ulianza
kuharibika mwaka 2009, baada ya Slaa kuwa na mahusiano na mwanamke mwingine kinyume cha sheria. "Tangu mwaka huo 2009, Slaa
akaitelekeza familia yake kwa kutoipatia huduma," imeeleza hati hiyo.
Kamili anaiomba
mahakama iamuru kuwa yeye na Slaa bado ni mke na mume na kwamba
Mushumbusi aliingilia ndoa yao hivyo mahakama izuie ndoa inayotajiwa
kufungwa Julai 21, mwaka huu huko Karatu
mkoani Manyara.
Kamili pia amewasilisha hati hiyo ya mashtaka kwa Kiongozi
Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo.
Kamili akamweleza askofu mkuu huyo wa jimbo Katoliki la Dar
es Salaam, kuwa moja ya Parokia za Dar es Salaam zina taarifa ya ndoa hiyo.
Nakala ya madai hayo pia imewasilishwa kwa msajili wa
Mahakama Kuu, Msajili wa ndoa na kwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Mbulu.
No comments:
Post a Comment