Monday, July 9, 2012

MBUNGE CCM ACHENJIA WABUNGE WENZAKE, ATAKA WIZARA YA MAJI IFUTILIWE MBALI


Mhe. Ali Kessy Mohamed
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Mhe. Ali Kessy Mohamed, amewaponda wabunge wenzake wanaosimama bungeni na kulalamika kuwa majimbo yao hayana maji halafu mwishoni mwa michango yao wanaunga mkono kwa kupitisha ‘Mia kwa Mia’ bajeti ya Wizara ya Maji.

Mhe. Kessy aliyeonekana kuongea kwa hisia kali huku akishangiliwa mfululizo na wenzake bungeni leo jioni, alitaka Wizara ya Maji ifumuliwe kwani haionekani kuwa na uwezo wa kumaliza tatizo la maji ambayo ni uhai.  

Mbunge huyo aliongeza kuwa inashangaza kuona kuwa wakati wa awamu ya kwanza (ya Rais Nyerere), maji yalikuwa si tatizo kubwa nchini; lakini hivi sasa hali imekuwa ngumu zaidi, ingawa kuna wizara maalum ya kushughulikia maji peke yake badala ya enzi hizo ambako iliwekwa pamoja na nishati na madini.

Alisema inasikitisha zaidi kuona kuwa tafiti zilizopo hadi sasa zinaonyesha kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya maji safi ya ardhini kuliko nchi zote barani Afrika, lakini maeneo mengi nchini hayana maji.

Aliongeza kuwa hivi sasa kuna Sh. bilioni 300 zimefichwa na watu Uswisi, nyingine zinatajwa kuwa ni Sh. Trilioni 11,  lakini inasikitisha kuona kuwa hadi leo hii bado maeneo mengi hayana maji na hakuna hatua za dhati zinazochukuliwa kukomesha tatizo hili.    
“Mimi nimekaa Namanyere siku tatu bila kuoga kwa sababu hakuna maji… mimi ni mwanaume, je kwa wanawake hali inakuwaje?”

“Na wewe spika (Naibu Spika Job Ndugai) usiunge mkono hoja, ukiunga mkono utakuwa hujawatendea haki wanawake wa jimbo lako (la Kongwa),” alisema.   

“Mimi siungi mkono hoja hii… naomba na wengine waipinge na wamnanchi wawakatae wabunge wanaoipitisha huku wakijua majimbo yao hayana maji,” alisema Mhe. Kessy.    

No comments:

Post a Comment