Jose Mourinho |
MADRID, Hispania
BARCELONA wamepinga vikali uamuzi wa
Shirikisho la Soka la Hispania kufuta adhabu ya kifungo cha mechi mbili iliyokuwa
ikimkabili kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho kwa kosa la kumtia kidole cha
macho msimu uliopita aliyekuwa kocha msaidizi wa Barca, Tito Vilanova.
Ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja sasa
kabla ya kuanza kwa msimu wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania 2012-13 La Liga, tayari
‘bifu’ kali limeanza baina ya mahasimu hao wa jadi.
Msemaji wa Barca, Toni Freixa amesema
kwamba msamaha aliopewa Mourinho, ikiwa ni sehemu ya misamaha ya jumla iliyotolewa
kwa wachezaji na makocha, unaharibu picha ya soka la Hispania na pia unachochea
zaidi kufanyika kwa vitendo vingine vya aina hiyo.
Mourinho alipewa adhabu ya kufungiwa
baada ya kumtovuga Vilanova, ambaye sasa ndiye kocha wa Barcelona aliyerithi
mikoba ya kocha aliyekataa kusaini mkataba mpya, Pep Guardiola. Vilanova pia
amenufaika na msamaha huo kwani pia alikuwa akikabiliwa na adhabu ya kufungiwa
mechi moja kwa kosa la kujibu mapigo ya Mourinho.
Freixa amesema kuwa rais wa Barca,
Sandro Rosell ameelezea kutofurahishwa kwa klabu yao kufuatia msamaha alioupata
Mourinho baada ya adhabu kuondolewa kwenye mkutano wa bodi ya shirikisho la
soka uliofanyika jana mjini Madrid.
"Kadri tunavyoelewa, shambulizi dhidi
ya kocha linastahili adhabu," Freixa alisema kupitia tovuti ya Barca
(www.fcbarcelona.com).
"Uamuzi huu hauna maana kwamba mgomvi
hana hatia, lakini unafanya waamini kwamba wanaweza kuendelea kushambulia watu
wengine bila kuwa na hofu ya kuadhibiwa," aliongeza.
"Si mfano mzuri kwa soka la
Hispania ikiwa kosa hili litapita bila ya kaudhibiwa."
No comments:
Post a Comment