Tuesday, July 10, 2012

CAPELLO, GUARDIOLA WATAJWA ORODHA YA MAKOCHA WANAOTAKIWA TAIFA URUSI

Pep Guardiola

Fabio Capello

Harry Redknapp

Rafa Benitez

MOSCOW, Urusi
KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya England, Fabio Capello na kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola ni miongoni mwa makocha maarufu 13 waliopewa nafasi za juu kutwaa nafasi ya kuifundisha timu ya taifa ya Urusi, Chama cha Soka cha Urusi (RFU) kimesema leo.

Orodha hiyo pia inawahsisha kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur, Harry Redknapp, kocha wa zamani wa Liverpool, Rafael Benitez, kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Italia, Marcello Lippi na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Argentina, Marcelo Bielsa.

"RFU inapenda kutangaza rasmi kwamba imepanga kuzungumza na wataalam hawa ili mmoja kati yao awe kocha mkuu wa timu ya taifa ya Urusi," chama hicho kilisema katika taarifa yake fupi kupitia tovuti yao (www.rfs.ru).

Phil Smith, wakala wa Redknapp, alisema kwamba mteja wake yuko wazi kwa majadiliano kuhusiana na mpango huo.

"Haswaa," Smith alikaririwa akisema katika vyombo vya habari vya Urusi wakati alipoulizwa kama Redknapp, aliyetimuliwa na Tottenham mwezi uliopita, atakuwa tayari kutwaa kibarua hicho.

"Je, Harry atasita kuja Urusi? Hapana. Yuko tayari kwenda na kuishi katika nchi yoyote, hasa nchi kubwa kama Urusi. Nadhani ikija ofa kama hiyo itamvutia tu, lakini hadi sasa, hatujasikia chochote kuhusiana na jambo hilo."

Kocha mmoja tu ambaye haishangazi ni kwanini hajaonekana kwenye orodha hiyo ni wa Manchester City, Muitalia Roberto Mancini, ambaye amekubali kusaini mkataba mpya wa miaka mitano wa kuifundisha klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England jana.

Jana, vyombo vya habari vya Urusi, vilikariri vyanzo kutoka RFU na Wizara ya Michezo, vikisema kwamba Mancini alikubali kusaini mkataba wa miaka minne kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Urusi baada ya maafisa kukuta "mkataba uliosaniwa" katika kabati la bosi wa zamani wa RFU, Sergei Fursenko.

Fursenko, rafiki wa karibu wa Waziri Mkuu wa Urusi, Vladimir Putin, aliamua kubwaga manyanga mwezi uliopita.

UTANI
RFU ililazimika kufichua majina ya makocha wanaowafukuzia kufuatia uvumi mkali unaoenezwa na vyombo vya habari kuhusiana na nafasi hiyo baada ya kuondoka kwa Mholanzi Dick Advocaat kufuatia kutolewa ‘kuchemsha’ kwa Urusi kwenye hatua ya makundi ya fainali za Euro 2012.

Wengine katika orodha ya RFU ni Warusi Valery Gazzayev, Anatoly Byshovets na Yuri Semin, ambao waliwahi kuifundisha timu hiyo katika miaka ya nyuma lakini wakatimuliwa au kujiuzulu kufuatia matokeo mabaya waliyopata.

Kocha wa zamani wa CSKA Moscow, Gazzayev na Valery Nepomnyashchy, aliyeiongoza Cameroon na kuifikisha katika robo fainali ya Kombe la Dunia Mwaka 1990, aliita mchakato huo kuwa ni utani.

"Huu ni utani na mimi sina la kusema," Gazzayev alikaririwa na gazeti la Sovietsky Sport, wakati Nepomnyashchy mwenye miaka 68 alisema: "Jina langu liko kwenye orodha? Sawa, lakini ni lazima huo utakuwa ni utani tu."

No comments:

Post a Comment