*BABAKE MDOGO, SHANGAZI, BABU WAMUOMBA AENDE GHANA WALAU KUWASALIMIA TU
Baadhi ya ndugu wa Kibaiolojia wa Balotelli walioko Ghana |
Namna hii Balotelli atarudi Ghana kweli? Afuate nini? Hapa ni katika pozi lake mojawapo la kula bata na vimwana akiwa majuu |
Balotelli akiwa amevalia aina ya kofia ambayo aliwahi kumtumia baba yake mkubwa nchini Ghana na kuambatanisha na zawadi nyingine alizoanguka saini yake. |
ACCRA, Ghana
Ndugu wa kifamilia nchini Ghana wa straika
waManchester City, Mario Balotelli ameungana
na maombi yaliyotolewa na wazazi wa kibaiolojia wa mchezaji huyo kumtaka arudi
kwao mara moja.
Mario ni straika wa bei mbaya ambaye
thamani yake ya sasa sokoni imepanda hadi kufikia paundi za England milioni 52
na ingawa alizaliwa Agosti 12, 1990 na wazazi Waghana, Rose na Thomas Barwuah, aliasiliwa
na kulelewa na wazazi wake wa sasa wa Italia wakati akiwa na miaka mitatu kwa
sababu ya matatizo ya kiafya aliyokuwa nayo. Alizaliwa mjini Palermo, kusini
mwa Italia.
Hadi sasa kuna simulizi za aina mbili
kuhusiana na namna Mario alivyochukuliwa na kulelewa na wazazi wake wa kurithi
-- familia ya Muitalia Balotelli.
Mario alisema katika mahojiano yake
kwamba alitelekezwa hospitalini na wazazi wake wa kibaiolojia, wa familia ya Barwuah.
Hata hivyo, Mzee Barwuah na mkewe
wamekanusha madai hayo na kusisitiza kwamba, kilichotokea ni kuwa wao hawakuwa
na fedha za kulipia ‘bili’ kubwa ya gharama za hospitali zilizotokana na
matibabu yake, na kwamba, familia ya Balotelli ikatoa ofa ya kumtwaa kwa muda ili
kumlea lakini kinyume chake hawakumrejesha na kumtwaa jumla.
“Kwanza hatukuwa na uhakika, lakini baadaye
tukakubali kwa kuamini kwamba pengine uamuzi wao utakuwa na faida kwa Mario. Tulimuona
kila wiki na kila kitu kilienda vizuri.
“Tulidhani kwamba kuna wakati, baada
ya matatizo kwisha, Mario angerudi mikononi mwetu.
Lakini badala yake, kila mara tulipojaribu
kumrudisha, familia ya Balotelli ikawa ikiongeza muda wa kutaka kuwa naye,” Mr.
Barwuah aliliambia Daily Mail la Uingereza.
Tangu wakati huo, familia ya Barwuah
imekuwa ikimsihi Mario kurejea mikononi mwao lakini kinyume chake akachukua
uraia wa Italia wakati alipotimiza miaka 18 na mwishowe kubadilisha jumla jina
la baba yake na kuwa Balotelli.
Mario amepuuza mwito wa ‘kurejea
nyumbani’ na badala yake ameendelea kuwa gumzo duniani kwa mambo mawili anayotambua
kwamba anayaweza sana: kucheza soka safi na kufanya mambo ‘kiukichaa’.
Hata hivyo, yapo matumaini kwa familia
ya Barwuah kama Daily Record lilivyoandika kwamba ndugu wa ukoo wa Mario mjini kwao
Konongo, Ghana, wameunga mkono kampeni ya kumsihi Mario arudi nyumbani ingawa wao
hawajawahi kumtia mchoni.
Taarifa hizo zimemnukuu Alex Barwuah,
30, baba mdogo wa Mario, akisema: “Wote tunajivunia sana kwa ajili yake.
Tulifurahi sana wakati alipofunga
mabao yote yaliyoipeleka Italia katika fainali ya michuano ya Euro 2012.Wakati
alipovua jezi na kuonyesha kifua chake baada ya kufunga goli, marafiki zangu
walinifanya na mimi nivue shati kama yeye.
Magoli yake yalinifanya nijihisi kuwa
karibu naye. Sijawahi kukutana na Mario lakini najisikia furaha sana ninapomuona
kwenye TV.
Huwa tunamtazama kadri inavyowezekana.
Najisikia fahari kwamba yeye ni mmoja wa wanafamilia yetu.
“Hata hivyo najisikia vibaya kwa
kutowahi kukutana naye, na kwamba baba yangu hajawahi kumuona mjukuu wake huyu …
baba yangu alikuwa akitazama kila mechi inayomuonyesha Mario na pia kuwa na
hamu sana ya kukutana naye, lakini haikuwezekana … naamini kwamba sasa Mario atakuja
kuonana na sisi na kujifunza mambo ya mababu zake.”
Baba mkubwa wa Mario, Nana, dereva
mstaafu wa mabasi, alifariki dunia hivi karibuni. Mario aliwahi mara moja
kumpelekea zawadi ya kofia ya ‘baseball’ iliyokuwa na saini yake.
Taarifa pia zimesema kwamba Kwaku
Awuah, babu yake Balotelli kwa upande wa mama, pia anamtaka mjukuu wake aende ‘nyumbani’
kwao kuwaona.
Kwaku, 80, alisema: “Inasikitisha kuwa
na mjukuu nyota duniani lakini kutowahi kumtia machoni hata mara moja …
najisikia vibaya sana kila mara ninapomuona kwenye TV au kumsoma magazetini …sihitaji
fedha zake.
Ninachotaka ni kumwambia tu kwamba
arudi kwenye mizizi yake kwa sababu, kuna msemo usemao, hakuna sehemu nzuri
kama nyumbani kwako.”
Inaelezwa vilevile kuwa Akosua Osaa
Barwuah, shangazi yake Mario na dada wa baba yake Thomas, pia anasikitishwa
kuona kwamba hajawahi kukutana na mpwa wake.
“Najisikia vibaya kila mara
ninapomuona kwenye TV…kaka yangu Thomas ameniletea picha ya Mario wakati
alipokuwa na miaka mitatu.
Nina mpwa maarufu duniani ambaye
sijawahi kukutana naye maishani mwangu,” alisema.
No comments:
Post a Comment