YONDANI AWATOSA MASHABIKI YANGA
MASHABIKI wa klabu ya Yanga waliofika leo kwenye uwanja wao wa Kaunda jijini Dar es Salaam kwa nia ya kushuhudia utambulisho wa Kevin Yondan walijisumbua bure kwani beki huyo wa mahasimu wao wa jadi, Simba hakutokea asubuhi wala jioni.
Hali hiyo iliibua maswali lukuki kutoka kwa baadhi ya mashabiki ambao awali waliamini kwamba Yondan angefika leo na kufanya mazoezi na wenzake kama walivyotangaziwa awali na msemaji wa klabu yao, Louis Sendeu.
Jana, Sendeu alisema kwamba Yondan aliyerejea nchini juzi akitokea Msumbiji alikokuwa na timu ya taifa, Taifa Stars angeungana na wenzake leo na mashabiki kibao wakafika Kaunda ili kumshuhudia kwa mara ya kwanza akivaa 'uzi' wa klabu yao.
Hata hivyo, Yondan aliyedaiwa kusajiliwa Yanga kwa dau la Sh. milioni 30 hakutokea na kuzima ndoto za mashabiki wa 'Wanajangwani'.
Sendeu alisema baadaye kwamba Yondan hakufika mazoezini kama walivyotarajia kwa vile yeye (Yondan) na wenzake waliokuwa na Stars Msumbiji wako mapumzikoni.
Waliokuwepo mazoezini jana ni pamoja na kipa Mustafa Barthez aliyetua juzi akitokea Simba, Said Bahanuzi na Juma Abdul waliotoka Mtibwa, Stansilaus Mbogo, Ibrahim Job, Seif Kijiko, Shamte Ally, Athuman Idd 'Chuji', Omega Seme, Rashid Idrissa, Jerryson Tegete, Nadir Haroub 'Cannavaro' na Nizar Khalfan.
Kocha Fred Felix Minziro ndiye aliyesimamia mazoezi hayo jana ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao ya kutetea taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) litakaloshindaniwa jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 14.
--------
No comments:
Post a Comment