RONALDO AIPELEKA URENO NUSU FAINALI , WAISUBIRI HISPANIA, UFARANSA
Goooooo....! Cristiano
Ronaldo wa Ureno (wa chini kushoto) akifunga goli dhidi ya Jamhuri ya Czech wakati wa mechi yao ya robo fainali ya
Euro 2012 kwenye Uwanja wa Taifa mjini Warsaw, leo usiku.
|
CRISTIANO Ronaldo alifunga bao safi la kichwa na kuipa Ureno ushindi wa 1-0 dhidi ya Jamhuri ya Czech leo usiku na kutinga nusu fainali ya Euro 2012 ambapo sasa watakutana na mshindi wa robo fainali nyingine itakayochezwa Jumamosi kati ya Hispania na Ufaransa.
Ureno walitawala mchezo katika mechi yao ya tano mfululizo ya robo fainali ya michuano hiyo ya Ulaya na nahodha wao Ronaldo aligongesha mwamba katika kila kipindi wakati akionyesha tena kiwango chake cha juu cha uchezaji.
Czechs walijilinda vyema na kuokolewa mara kadhaa na kipa wao Petr Cech kabla Ronaldo hajamtoroka beki aliyekuwa akimchunga na kuiwahi krosi ya Joao Moutinho kwa kupiga kichwa ‘kikali’ kilichokwenda moja kwa moja wavuni wakati zikiwa zimebaki dakika 10 kabla ya kumalizika kwa muda wa kawaida.
Hilo lilikuwa ni goli la tatu kufungwa katika fainali za Euro 2012 na mwanasoka huyo bora wa zamani wa Dunia baada ya kufunga pia mabao yote yaliyowapa ushindi wa 2-1 katika mechi yao iliyopita ya hatua ya makundi dhidi ya Uholanzi ambayo iliwapa nafasi ya kufuzu kwa hatua ya robo fainali kutoka kundi lao la B lililoongozwa na Ujerumani.
Katika robo fainali nyingine itakayochezwa kesho Ijumaa kuanzia saa 3:45 usiku, Ujerumani watavaana na Ugiriki.
---------
No comments:
Post a Comment