HISPANIA WAMHOFIA RIBERY
Ribery akijifua na wenzake leo kabla ya kutoka nje akichechemea |
GNIEWINO,
Poland
Kiwango
cha Alvaro Arbeloa katika fainali za Euro 2012 kimekuwa kikipondwa nyumbani
kwao Hispania na Ufaransa wanatarajiwa kumtumia winga wao hatari, Franck Ribery
kutumia udhaifu huo wakati watakapovaana Jumamosi katika mechi yao ya robo
fainali.
Mara
kadhaa Arbeloa alionekana akiyumba katika nafasi yake ya beki wa kulia katika mechi
zote tatu za Hispania za Kundi C mjini Gdansk, hasa alipokumbana na
washambuliaji machahari kama Ribery ambao wana kasi na ujanja mwingi, hivyo kuibua
wito wa kumtaka kocha Vicente del Bosque amkalishe benchi na nafasi yake acheze
Juanfran.
Akicheza
kwa namna ya kushambulia zaidi na pia akiwa ngangari katika kuzuia, Juanfran anaelezewa
vilevile kuwa ni mzuri pia katika kupiga krosi ‘kali’ zaidi ya Arbeloa, jambo
ambalo linaweza kumlazimisha Ribery ashuke ili asaidie ulinzi.
Hata
hivyo, Del Bosque haelekei kuwa tayari kucheza kamari kwa mchezaji ambaye ndio
kwanza alianza kuichezea Hispania mwishoni mwa Mei na hivyo ni wazi kwamba
ataendelea kumuamini Arbeloa, ambaye anajiandaa kucheza mechi ya 39 kwa timu yake
ya taifa mjini Donetsk Jumamosi.
Kwenye
mkutano na waandishi wa habari katika kambi ya Hispania mjini Gniewino, kaskazini
mwa Poland leo, Juanfran aliunga mkono Arbeloa acheze, lakini akaongeza kwamba naye
yuko tayari kucheza wakati wowote atakapohitajika.
"Yeye
ni mchezaji mwenzagu na nitamtetea mpaka kufa," beki huyo mwenye miaka 27
alisema.
"Hivi
sasa kocha anamuamini Alvaro na mimi ninaheshimu sana maamuzi yake," aliongeza.
"Ninamuamini
na pia kikosi timu nzima inamuamini. Kwa mtazamo wangu amecheza vizuri katika
hatua ya makundi na pia alikuwa na msimu mzuri sana kwenye klabu yake ya Real
Madrid."
RIBERY ‘NOMA’
Juanfran |
Arbeloa |
Ribery
alitoka nje ya uwanja wao wa mazoezi huku akichechemea jana Jumatano kutokana
na uvimbe , lakini msemaji wa timu alisema kwamba atakuwa ‘fiti’ wakati
Ufaransa ikijaribu kulinda rekodi yao ya kutowahi kufungwa na Hispania katika mechi
za mashindano, ikishinda tano na kupata sare moja.
"Kila
wakati (Ribery) anaweza kutengeneza nafasi ya kufunga kwa ajili yake mwenyewe
au kutoa pasi ya goli," Juanfran alisema.
"Ni
miongoni mwa wachezaji nyota wa Ufaransa na tunachotaka ni kuona kuwa hana siku
nzuri na pia kuona kwamba tunamudu kumzuia yeye na wahsambuliaji wenzake."
No comments:
Post a Comment