Casillas |
Ronaldo |
GNIEWINO, Poland
NAHODHA wa timu ya taifa ya Hispania,
kipa Iker Casillas amesema kuwa mshambuliaji Cristiano Ronaldo wa Ureno bado
hajaonyesha kiwango chake alichoonyesha msimu uliomalizika katika klabu
anayocheza naye pamoja ya Real Madrid.
Casillas ambaye anafukuzia rekodi ya
ushindi wa 100 akiwa na jezi ya Hispania wakati watakapocheza dhidi ya Ureno
katika nusu fainali ya kwanza ya Euro 2012 kesho, alisema kwamba kwa mtazamo
wake, Ronaldo aliyeifikisha Ureno nusu fainali kutokana na mabao matatu
yaliyomuweka kileleni mwa orodha ya wafungaji wa michuano hiyo hadi sasa si
yule aliyetisha Real Madrid na kuwapa ubingwa wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania
kwa mara ya kwanza baada ya miaka minne.
"Alikuwa na msimu mzuri Real
Madrid kutokana na namna alivyocheza, mabao aliyofunga na rekodi
alizoweka," kipa huyo mwenye miaka 31, anayefahamika zaidi Hispania kama
"Saint Iker" kutokana na uwezo wake wa kuokoa kiajabu michomo ya
hatari kutoka karibu na lango, alikaririwa akisema juzi na katika gazeti la
michezo la kila siku la Marca.
"Sidhani kama hivi sasa anacheza
katika kiwango chake cha juu," aliongeza.
Ronaldo amekuwa mhimili wa Ureno
kutokana na kasi yake inayosumbua mabeki wa upinzani na pia mabao
yaliyoifikisha Ureno katika hatua ya nusu fainali ya Euro 2012.
No comments:
Post a Comment