Olivier Giroud |
LONDON, England
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Ufaransa,
Olivier Giroud amejiunga na Arsenal kwa mkataba wa muda mrefu, klabu hiyo ya
Ligi Kuu ya England ilisema leo.
Mchezaji huyo mwenye miaka 25
alikamilisha kuchukuliwa vipimo vya afya kwenye klabu hiyo juzi na kukubaliana
na yaliyomo katika mkataba wake utakaoanza rasmi Julai Mosi, Arsenal iliongeza
katika taarifa waliyotoa kupitia tovuti yao (www.arsenal.com)
"Kukamilika kwa uhamisho wake
sasa ni suala tu la utaratibu wa mchakato wenyewe," iliongeza klabu hiyo
ya jiji la London, iliyomaliza kwenye nafasi ya tatu katika Ligi Kuu ya England
msimu uliopita na kutwaa nafasi ya kucheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Giroud ametua Arsenal akitokea kwa
mabingwa wa Ufaransa, Montpellier baada ya kuichezea timu ya taifa lake katika fainali
za Euro 2012 nchini Poland na Ukraine.
Mabao yake 21 katika mechi 36
yalimfanya amalize kileleni mwa orodha ya wafungaji wa Ligue 1, Ligi Kuu ya
Ufaransa msimu uliopita akiwa pamoja na Nene wa klabu ya Paris St Germain.
"Tumefurahi kumsajili Olivier
Giroud," alisema kocha wa Arsenal, Mfaransa Arsene Wenger.
"Ana umbile zuri la soka, ni
mkali wa mipira ya juu na pia hucheza kwa kujituma.
"Tunayo furaha kubwa kuhusiana na
Olivier kujiunga nasi na ataongeza idadi ya washambuliaji tunaoweza kuwatumia
msimu ujao."
Giroud alisema kwamba ndoto yake
ilikuwa ni kucheza katika Ligi Kuu ya England na alivutiwa na Arsenal kutokana
na falsafa yao ya soka na pia umaarufu wa Wenger.
No comments:
Post a Comment