Mario Balotelli na Antonio Cassano wakitembea wakati wa mazoezi ya timu ya taifa ya Italia mjini Krakow, Poland jana. |
GAZETI la kila siku linaloongoza Italia la Gazzetta dello Sport limeomba radhi kwa kuchapisha katuni inayomfananisha mchezaji mweusi wa timu ya taifa ya Italia, Mario Balotelli, na sokwe mkubwa wa kwenye filamu ya King Kong.
Kasha la filamu ya King Kong likimuonyesha mnyama huyo mkubwa wa kufikirika. |
Katuni ya mshambuliaji huyo wa Manchester City, ililenga kumuonyesha kama shujaa mkubwa aliyeteka England.
Hata hivyo, kuamkia mechi ya ushindi wa Italia ya robo fainali ya Euro 2012 dhidi ya England na kuelekea nusu fainali dhidi ya Ujerumani Alhamisi, katuni hiyo imepata malalamiko kutoka kwa wasomaji.
"Tunathubutu kusema kwamba si moja ya kazi nzuri za mchora katuni wetu gwiji," Gazzetta lilisema.
"Kama mtu anaona inamuumiza tunaomba samahani.
"Gazeti hili daima limekuwa likipambana dhidi ya ubaguzi wa rangi viwanjani na kupinga sauti za nyani anazoelekezewa Balotelli."
Si Balotteli wala timu ya taifa ya Italia walipatikana kutoa maoni yao.
Katuni hiyo iliyochapishwa katika toleo la Jumapili awali ilipita bila ya kubainika lakini sasa imegeuka gumzo kubwa kote kwenye Internet.
Balotelli, mzaliwa wa Italia mwenye asili ya Ghana, alifanyiwa ubaguzi na mashabiki wa Juventus wakati akiichezea Inter Milan na klabu hiyo ya Turin iliadhibiwa kucheza mechi ya Serie A katika uwanja usio na mashabiki.
No comments:
Post a Comment