Thursday, June 28, 2012

FABREGAS AIPELEKA HISPANIA FAINALI EURO 2012

Fabregas akishangilia penati yake ambayo iliwapeleka Hispania katika fainali ya Euro 2012

Casillas akipangua penati ya Ureno 

Aiya weee...! Ronaldo akionyesha kusikitika baada ya Bruno Alves kukosa penati yao kabla Fabregas hajafunga penati iliyowapa ushindi Hispania

Wachezaji wa Hispania wakishangilia baada ya kuifunga Ureno katika mechi yao ya nusu fainali ya Euro 2012 kwenye Uwanja wa Donbass Arena mjini Donetsk.  




DONETSK, Ukraine
MTOKEA benchi Cesc Fabregas alipiga penati iliyowapa goli la ushindi wakati mabingwa watetezi, Hispania wakiifunga Ureno kwa penati 4-2 baada ya sare ya awali ya 0-0 katika dakika 120 za nusu fainali yao ya Euro 2012 jana usiku.

Kipa wa Hispania, Iker Casillas alipangua penati ya kwanza ya Joao Moutinho kabla Bruno Alves hajagongesha ‘besela’ na kumpa nafasi mtokea benchi Fabregas kufunga bao la ushindi kwa penati iliyogonga mlingoti wa goli kabla ya kujaa wavuni.

Baada ya mechi kali ya kipindi cha kwanza wakati Ureno wakiwabana majirani zao, kukatokea nafasi chache za kufunga ikiwa ni pamoja na mashuti mawili ya ‘fri-kiki’ ya Cristiano Ronaldo yaliyopaa juu ya lango na jingine la dakika ya mwisho alilopaisha vilevile baada ya kufanya shambulizi la kustukiza.

Alvaro Arbeloa wa Hispania alipiga shuti lililopaa katika dakika ya tisa ikiwa ni nafasi nzuri zaidi kwa kikosi chao kilichokosa uelewano hadi Andres Iniesta alipomlazimisha kipa Rui Patricio kufanya kazi ya ziada kuokoa shuti lililokuwa likielekea langoni kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza cha muda wa nyongeza na mwishowe wakaongeza kasi yao na kutawala mechi.

Fabregas alifunga pia penati ya mwisho ya Hispania iliyoivusha katika hatua ya robo fainali ya Euro 2008 dhidi ya Italia kabla baadaye kutwaa ubingwa huo.

Ujerumani watacheza dhidi ya Italia mjini Warsaw leo katika mechi nyingine ya nusu fainali ambapo washindi watacheza Jumapili mjini Kiev katika fainali dhidi ya Hispania.

----

2 comments:

  1. Big up Spain kwa kuvuka kigingi, ila wajipange vizuri kwa fainali... Haitakuwa ya kitoto, jana wali-struggle at times kuwapenya Wareno

    ReplyDelete
  2. Ni nafasi ya kutengeneza historia nyingine kwa Waspaniola...

    ReplyDelete