Tuesday, June 26, 2012
EBSS SASA YATUA LINDI JUMAMOSI
Na Mwandishi Wetu
SHINDANO kubwa la kusaka na kuendeleza vipaji vya kuimba nchini la Epiq Bongo Stars Search Jumamosi hii litakuwa mkoani Lindi katika ukumbi wa Police Officers Mess, taarifa ya waandaaji ilisema jana.
Washiriki watafanyiwa usaili kuanzia saa moja asubuhi kabla ya kuanza kuonyesha vipaji vyao mbele ya majaji, iliongeza taarifa hiyo.
Jaji Mkuu wa EBSS, Ritha Paulsen alisema kwamba kama ilivyokuwa katika mkoa wa Dodoma na kisiwani Zanzibar, wanatarajia kupata vipaji lukuki mkoani Lindi na akawasihi wasichana kujitokeza kwa wingi.
"Mimi ninaamini kuwa mkoa wa Lindi una vipaji vingi. Yaani kama tulivyoona kwenye maeneo mengine, nadhani Lindi kutakuwa na ushindani mkali kwa sababu wapo baadhi ya wasanii kutoka Lindi ambao wamefanya vyema katika medani ya muziki nchini," alisema Ritha.
Akizungumzia washindi waliopatikana Dodoma na Zanzibar, Ritha alisema kuwa wamekuwa wakiimba vizuri na walionehsa uwezo mkubwa katika kupangilia sauti zao.
Naye Mkuu wa Mawasiliano wa Zantel, Awaichi Mawalla alisema kuwa Zantel ikiwa kama mdhamini mkuu wa EBSS 2012, wanaamini kuwa wakazi wa Lindi watajitokeza kwa wingi na kuleta ushindani mkubwa katika mashindano hayo.
Vijana 10 wamepatikana kutoka Dodoma na Zanzibar tangu msimu huu wa EBSS ulipoanza.
Labels:
Burudani
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment