*Sasa ataka ufungaji bora, vinara kabaki yeye tu
MSHAMBULIAJI wa Manchester City, Mario Balotelli alivutiwa na kiwango chake katika ushindi wa Italia wa 2-1 dhidi ya Ujerumani katika nusu fainali ya Euro 2012 usiku wa jana.
Balotelli alifunga magoli mawili "makali" yaliyoendeleza unyonge wa Ujerumani kwa Waitalia. Ujerumani hawajawafunga Italia kwa nusu karne iliyopita.
"Mwisho wa mechi nilienda kwa mama yangu, kile kilikuwa kipindi bora kabisa. Nilimweleza kuwa magoli yake yalikuwa ni kwa ajili yake,” alisema.
"Nimeisubiri siku hii kwa muda mrefu sana, hasa kwa sababu mama yangu si mdogo tena na hawezi kusafiri mbali, hivyo ninapaswa kumpa furaha anapokuwa amesafiri umbali wote hadi hapa. Baba yangu atakuwepo mjini Kiev kwa ajili ya fainali pia.
"Kabla ya mechi walikuwepo mama yangu, kaka zangu, shemeji yangu na rafiki yangu mkubwa wote pembeni ya uwanja. Uwepo wao jirani yangu kiasi kile, ulinipa mizuka. Muziki gani huwa nasikiliza kabla ya mechi? Drake. Yeye ni rafiki yangu."
Kutokana na magoli hayo mawili, Balotelli amefikisha jumla ya mabao yake kwenye Euro 2012 kuwa matatu akiungana na vinara wa mabao, lakini ni yeye pekee aliyebaki kwenye michuano, hivyo ana nafasi kubwa ya kuwa mfungaji bora.
"Nitajaribu kushinda tuzo ya mfungaji bora. Katika soka wakati mwingine unaweza kujaribu mara nyingi na mpira usiende wavuni, au ukajaribu mara chache na mpira ukatinga wavuni mara zote.
"Ilikuwa ni bonge la pasi, la aina ambayo ni Antonio Cassano pekee anaweza kuitoa, wakati pasi ya Riccardo Montolivo ilikuwa kali sana pia. Nilishangilia? Ndio nilisema ningeshangilia."
No comments:
Post a Comment