Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
AZAM
juzi ilitetea Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga Tusker FC ya Kenya
mabao 2-1 ndani ya dakika 120 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, bao lao
la ushindi likifungwa na Gaudence Exavery Mwaikimba. Je, wajua mabao 10
ambayo amefunga mshambuliaji huyo na hatayasahau daima maishani mwake?
Endelea.
10.
Ilikuwa ni katika fainali ya Kombe la Mapinduzi mwaka 2013 kwenye
Uwanja wa Amaan Zanzibar, wakati Gaudence alipopokea pasi ya Brian Umony
na kuwahadaa mabeki wa Tusker FC ya Kenya, kabla ya kufumua shuti kali
lililotinga nyavuni. Anasema hatalisahau bao hili kwa sababu liliipa
timu yake, Azam FC Kombe la Mapinduzi naye akitoka uwanjani kama shujaa
wa mchezo.
9.
Ilikuwa ni katika fainali ya Kombe la Taifa mwaka 2005, akichezea timu
ya mkoa wa Mbeya, wakati alipowazidi nguvu na maarifa mabeki wa Mtwara
kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na kuifungia Mbeya bao la pili na
la ushindi ndani ya dakika 30 za nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika
kwa sare ya 1-1. Anasema hatalisahau bao hili, kwa sababu liliipa Kombe
Mbeya na kumjengea yeye heshima nyumbani, kama mmoja wa wanasoka wakubwa
waliowahi kutokea Mbeya.
8.
Ilikuwa ni katika fainali ya Kombe la Taifa mwaka 2011 dhidi ya Mwanza,
kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha alipoifungia Mbeya bao
pekee la ushindi dakika za majeruhi baada ya kutimu dakika 90 za kawaida
za mchezo. Anasema hawezi kulisahau bao hilo, kwa sababu lilimuwezesha
pia kuibuka mfungaji bora wa mashindano hayo na kuzidi kujijengea
heshima Mbeya.
7.
Ilikuwa ni katika Ligi Kuu ya Bara mwaka 2005 akiichezea Ashanti United
ya Ilala, Dar es Salaam alipoinusuru kuzama mbele ya Yanga kwenye
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha baada ya kuifungia bao la
kusawazisha na kuwakatili Watoto wa Jangwani kuondoka na pointi tatu.
Anasema analikumbuka bao hilo kwa sababu ni kama lilimfungulia njia ya
kusajiliwa Yanga, kwani tangu siku hiyo ndipo viongozi wa timu hiyo
walipoanza kuzungumza naye, hatimaye wakamsajili 2006.
6.
Ilikuwa ni mwaka 2007 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, kati ya
Tanzania, Taifa Stars chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo alipoifungia
bao Stars lililoelekea kuwa la ushindi dhidi ya Angola Uwanja wa Uhuru,
Dar es Salaam, kabla ya mshambuliaji wa zamani wa Manchester United ya
England, Manucho kuisawazishia Angola. Anasema analikumbuka bao hilo kwa
sababu lilimjengea heshima katika medani ya kimataifa, kwa sababu
Angola wakati huo ilikuwa imetoka kucheza Kombe la Dunia mwaka 2006
nchini Ujerumani.
5.
Ilikuwa ni mwaka 2006 kwenye michuano ya Kombe la Tusker, wakati
Gaudence Mwaikimba alipovunja mtego wa kuotea wa mabeki wa Moro United
na kumtungua kipa Amani Simba, kuifungia Yanga bao la pili akitoka
kufunga pia la kwanza. Anasema analikumbuka bao la pili kwa sababu,
baada ya kufunga Moro United waligomea mechi na mchezo ukaishia hapo,
Yanga ikitinga Nusu Fainali.
4.
Ilikuwa ni mwaka 2012 katika siku zake za mwanzoni kabisa Azam, wakati
alipoifungia timu hiyo bao la ushindi kwenye Nusu Fainali ya Kombe la
Mapinduzi dhidi ya Simba SC Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika dakika za
mwishoni kabisa za mchezo wakishinda 2-1. Anasema analikumbuka bao hilo
kwa sababu liliipeleka Azam fainali ya michuano hiyo, ambako
walifanikiwa kutwaa Kombe la kwanza katika historia ya timu hiyo.
3.
Ilikuwa ni mwaka 2006 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya
Tanzania na Rwanda wakati Gaudence Mwaikimba alipofunga bao pekee la
ushindi timu ikiwa chini ya kocha Dk. Mshindo Msolla. Anasema hawezi
kulisahau bao hilo kwa sababu siku hiyo ndiyo kocha Mbrazil, Marcio
Maximo alikuwa amewasili nchini na alikuwa jukwaani akiangalia
wachezaji, hivyo kufanya kwake vizuri kulimfanya aendelee kuwa timu ya
taifa chini ya kocha huyo wa Kibrazil.
2.
Ilikuwa ni mwaka 2007 katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki
na Kati, Kombe la Kagame wakati Mwaikimba alipoifungia Yanga bao la
kwanza kati ya mawili ya kusawazisha, la pili likifungwa na Mkenya Ben
Mwalala hivyo kufanya sare ya 2-2. Anasema analikumbuka bao hilo kwa
sababu liliirudisha timu yao mchezoni ikitoka nyuma kwa 2-0 na kupata
sare ya 2-2 hivyo kuingia Robo Fainali ya michuano hiyo mjini Kigali,
Rwanda.
1.ilikuwa
ni mwaka 2006 katika msimu wake wa kwanza kwenye klabu ya Yanga,
Mwaikimba alipoifungia Yanga bao la tatu, baada ya kufunga mawili ya
awali pia katika mchezo wa Ligi Kuu ya Bara dhidi ya Ruvu Shooting
Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Anasema hatalisahau bao hilo kwa sababu
lilikamilisha hat-trick yake pekee katika Ligi Kuu kihistoria hadi sasa
na kufanya mashabiki warejee makwao siku hiyo wakiimba jina lake.
Naam, hayo ndio mabao 10 ambayo Gauedence anasema ataendelea kuyakumbuka daima kati ya mabao aliyowahi kufunga.
Mwaikimba, akishangilia moja ya mabao aliyofunga |
WASIFU WAKE:
JINA: Gaudence Exavery Mwaikimba
KUZALIWA: Oktoba 5, 1984
ALIPOZALIWA: Kyela, Mbeya
KLABU YAKE: Azam FC
KUJIUNGA: 2012
KLABU ZA AWALI:
Mwaka Klabu
2003-2004: Tukuyu Stars
2004- 2005: Kahama United
2005- 2006: Ashanti United
2006- 2009: Yanga SC
2009-2010: Sur (Oman)
2010: Prisons FC
2011- 2012: Kagera Sugar
2012: Moro United
2012 hadi sasa Azam FC
Mwaikimba akifurahia na mashabiki wake Kombe la Mapinduzi jana |
No comments:
Post a Comment