Tupaki basi wazee huyu noma... Lionel Messi akijaribu kushuti mbele ya "msitu" wa mabeki wa Malaga jana |
Cesc Fabregas wa Barcelona akishangilia goli la pili aliloifungia timu yake dhidi ya Malaga jana |
Napita humu humu... Kiungo wa Barcelona, Andres Iniesta (katikati) akizungukwa na "msitu" wa wachezaji wa Malaga jana. |
Isco wa Malaga akikokota ngoma huku akichungwa na Lione Messi wa Barca jana |
BARCELONA imemaliza mzunguko wa kwanza wa La Liga kwa rekodi mpya baada ya kushinda mechi 18 kati ya 19 walizocheza wakati walipoilaza timu iliyo katika kiwango cha juu ya Malaga kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Rosaleda jana usiku.
Ni rekodi ya aina yake katika La Liga ambapo ni rangi za Barcelona tu zinazotawala. Ni timu ya Real Madrid pekee iliyoweza kupata pointi kutoka kwa Barca katika mzunguko wa kwanza baada ya timu hizo kutoka sare. Barcelona sasa inaongoza kwa tofauti ya pointi 11 juu ya Atletico de Madrid, ambao ndiwo wanaoonekana angalau wanawakaribia vinara huku mahasimu Real Madrid wakiwa wameachwa kwa pointi 18 sasa.
Messi kwa mara nyingine tena alifunga goli jana. Lilikuwa ni bao lake la 27 la Ligi msimu huu baada ya kutumia makosa ya Ignacio Camacho kumrudishia pasi fupi kipa ambapo Messi aliuwahi akampiga chenga kipa Willy Caballero na kufunga goli la kuongoza katikamechi ambayo Malaga wangeweza kujisifu "kumtia mfukoni" mwanasoka bora wa dunia mara nne mfululizo, Messi.
Licha ya kutoonyesha makeke mengi huku akichungwa sana, Messi alimpikia Cesc Fabregas goli la pili na akampikia pia goli la tatu yosso Thiago Alcantara aliyeingia kutokea benchi. Malaga walipata goli lao la kufutia machozi katika dakika za lala salama kwa 'fri-kiki' matata sana iliyokwenda moja kwa moja wavuni kutoka kwa Muargentina, Diego Buonanotte.
Kocha raia wa Chile, Manuel Pellegrini, wa Malaga alisema kabla ya mechi hiyo kwamba walidhamiria kuilaza Barcelona kama walipoichama Real Madrid 3-2, lakini kwa muda mrefu walijikuta wakiusaka mpira kwa "tochi" kutoka Barca iliyokamilika.
Baada ya mechi hiyo, timu hizo zitakutana tena kwa mara ya pili keshokutwa Jumatano katika robo fainali ya Kombe la Mfalme kwenye Uwanja wa Camp Nou.
No comments:
Post a Comment