George Banda wa Yanga (kulia) akijaribu kuwatoka mabeki wa Tusker leo Desemba 26, 2012. |
Yanga iliwasononesha mashabiki wake katika siku ya
kukamilisha sherehe za sikukuu ya krismasi (boxing day) baada ya kubanwa kwa
muda mwingi na kukubali kipigo cha bao 1-0 katika mechi yao ya kirafiki dhidi
ya Tusker ya Kenya kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Wageni walifanya mashambulizi mengi na kutangulia kupata
goli walilostahili kwa njia ya penati katika dakika ya mwisho ya kipindi cha
kwanza baada ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kumuangusha Khalid Aucho wa Tusker
ndani ya ‘boksi’ na refa Israel Nkongo kuamuru penati iliyowekwa wavuni
kiufundi na Ismail Dunga.
Mashabiki wa Yanga walikuwa na wakati mgumu kutokana
na mashambulizi mengi zaidi kuelekea langoni mwao, lakini kipa kipa Ali Mustafa
‘Barthez” alifanya kazi kubwa ya kupunguza idadi ya mabao kwa kuokoa michomo
kadhaa ya hatari.
Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts alisema baada
ya mechi hiyo kuwa hakushangazwa na kipigo hicho kwani nyota wake kadhaa wa
kikosi cha kwanza hawakucheza, wakiwamo Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, Haruna
Niyinzima ‘Fabregas’ na kinara wa mabao katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu
ya Tanzania Bara, Didier Kavumbagu,
Hata hivyo, Kabange Twite ambaye ni pacha wa Mbuyu Twite aliyetua Yanga katika
kipindi cha usajili wa dirisha dogo alionyesha kiwango cha juu na kushangiliwa
kila mara kutokana na uchezaji wake wa ‘jihadi’ kuanzia mwanzo hadi mwisho wa
mechi.
Miongoni mwa nafasi chache walizopoteza Yanga ni
pamoja na dakika ya pili tu iliyopotezwa na George Banda, ‘tik-taka’ ya Said Bahanunzi iliyoparaza
kidogo ‘besela’ katika dakika ya 43 na kichwa cha Cannavaro kilichookolewa na
kipa Samwel; Odhiambo katika dakika ya 83.
Tusker walipoteza nafasi nyingi za kuongeza mabao
pia, zikiwamo za dakika ya sita na 34 kupitia kwa Dunga na dakika ya 86 wakati Edru
Sekayonga alipobaki na Barthez lakini akapiga shuti lililombabua usoni kipa
huyo na kumuumiza kiasi cha kufanya mechi isimame kwa dakika mbili ili atibiwe.
Kipigo cha jana ni cha pili kwa Yanga katika mechi
10 tangu Brandts aanze kuiongoza baada ya kurithi mikoba ya kocha
aliyetimuliwa, Mbelgiji Tom Saintfiet.
Hii ilikuwa
ni mechi ya pili Tusker ambao ni mabingwa wa Kenya, watateremka tena dimbani
mwishoni mwa wiki kucheza dhidi ya mabingwa wa Tanzania, Simba.
Vikosi:
Yanga:
Ally Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua/Simon
Msuva, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Ladislaus Mbogo/Stephano Mwasika, Nurdin
Bakar, Rehan Kibingu/Omega Seme, Kabange Twite, Said Bahanunzi, George Banda/Hamis
Kiiza, David Luhende.
Tusker:
Samwel Odhiambo, Luke Ochiend, Jeremial Bright, Mark
Odhiambo, Joseph Shikokoti, Khalid Aucho, Edwin Manono, Justine Monda, Ismail
Dunga/Edru Sekayonga (dk.46), Jesse Were/Andrew Tololwa, Robert Omonuki.
No comments:
Post a Comment