Na Ezekiel Kamwaga
MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Mhe; Ismail Aden Rage, amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa aliyekuwa msanii maarufu wa muziki na filamu, Hussein Ramadhani Mkiety, maarufu kwa jina la Sharo Milionea, kilichotokea jana usiku mkoani Tanga.
Kwa niaba ya klabu ya Simba na kwa niaba yake binafsi, Mwenyekiti anapenda kutuma salamu za pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote wa marehemu kutokana na msiba huu mkubwa sana si kwao pekee bali kwa taifa zima la Tanzania.
Sharo Milionea hakuwa msanii wa kawaida. Yeye ni miongoni mwa kizazi kipya cha vijana wa Kitanzania walioamua kutafuta maisha kwa kutumia vipaji walivyopewa na Mungu. Yeye alijitumbukiza zaidi katika uchekeshaji na baadaye akaonyesha uwezo mkubwa katika fani ya muziki.
Sharo alikuwa maarufu kiasi kwamba makampuni makubwa yalikuwa yameanza kumtumia kwenye matangazo yao ya kibiashara. Hii ilionyesha kwamba makampuni yalibaini faida itakayopatikana kwao kwa kumtumia msanii huyu ambaye bado alikuwa na heshima kubwa kwenye jamii kutokana na haiba yake na uwezo wake kwenye kazi alizokuwa akifanya.
Msiba huu umekuwa pigo kubwa kwa tasnia ya filamu ambayo bado inaomboleza vifo vya wasanii kama Steven Kanumba, Mlopelo na John Steven Maganga, waliofariki dunia mwaka huu pia.
"Ifahamike kwamba Sharo Milionea alikuwa miongoni mwa wasanii wa Kitanzania waliotuma maombi Simba ya kutaka kushiriki kwenye mchakato wa kutengeneza wimbo rasmi wa klabu ya Simba. Yeye alikuwa miongoni mwa wasanii waliokuwa wakiumizwa na ukweli kwamba klabu kama Simba inashindwa kufanya biashara ya kuuza nyimbo zake ilhali wanunuaji wapo," alisema Rage.
Kwa klabu ya Simba, namna pekee ya kumuenzi marehemu ni kufanyia kazi mambo ambayo alikuwa akitushauri kwenye eneo la biashara. Ni matumaini yetu kwamba iwapo tutafanya lile alilokuwa akitushauri, atakuwa mwenye amani huko alikotangulia mbele ya haki.
Rage amewaomba wasanii wa tasnia ya filamu na muziki kuwa watulivu na wenye subra kwenye kipindi hiki kigumu kwao. Kila kitu katika maisha ya wanadamu kinapangwa na Mwenyezi Mungu na ndiyo maana Waswahili wana msemo kuwa Kazi ya Mungu haina makosa.
Mola na ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Hussein Ramadhani Mkeity
(Kamwaga ni Ofisa Habari wa Simba SC).
No comments:
Post a Comment