Mwanamuziki JB Mpiana (waliokaa katikati) akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam |
NYOTA wa muziki wa dansi barani Afrika, JB Mpiana ametua jijini Dar es Salaam jana tayari kwa maonyesho kadhaa, likiwamo lile la uzinduzi wa albamu ya Mashujaa Band inayokwenda kwa jina la Risasi Kidole, litakalofanyika Ijumaa katika viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam.
Kabla ya shoo hiyo ya Ijumaa, JB Mpiana ambaye amekuja na kundi lake zima la Wenge Musica BCBG, likiwahusisha wanamuziki wake za zamani na wapya, atauwasha moto jijini Arusha kesho kabla ya kufanya kweli jijini Mwanza Jumapili.
Akizungumza katika Hoteli ya Double Tree iliyopo Masaki, Dar es Salaam, JB Mpiana ameahidi kutoa shoo ya aina yake ambayo anaamini itakonga nyoyo za Watanzania.
Alisema kuwa amefurahisa sana kuja Tanzania kwa mara nyingine, ikiwa ni pamoja na mapokezi aliyoyapata, akiahidi kutoa burudani ya nguvu kwa Watanzania kuwalipa mapokezi waliyomwonesha.
“Nina imani waandaaji wamefanya maandalizi ya kutosha, nimekuja na wanamuziki wangu wote 25, nimekuja na vifaa vyangu vyote vilivyopo katika kundi langu, ili kutoa burudani ya kutosha kwa Watanzania.
“Nimewaletea albamu inayojulikana kwa jina la Biloko (chakula), watanzania wajiandae kula, yaani kupata burudani ya nguvu kutoka kwangu na kundi langu,” alisema JB Mpiana.
Kati ya wasanii aliokuja nao, alisema wapo wale wa zamani aliokuwa nao enzi hizo ndani ya kundi lake hilo lilipoanza kutamba katika anga ya muziki, na wengine wapya ambao wapo fiti.
Katika programu yake hapa nchini, amesema atapiga nyimbo zake za zamani na mpya ili kuwapa watanzania fursa ya kupata vionjo vya zamani na vipya, kuweza kupima ubora wa kazi hizo.
Akizungumzia muziki wa Tanzania, amewataka wasanii wa hapa nchini kujituma na kuzipenda kazi zao na kuiheshimu waweze kufanikiwa katika kazi zao hizo.
Juu ya kiongozi wa safu ya unenguaji, alisema safari hii inaongozwa na mwanadada Zambrota, ikiwa ni baada ya kufariki kwa aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Monica.
“Nimefurahi sana kuja Tanzania kwa mara nyingine, wapenzi wa burudani wajiandae kupata shoo ya nguvu kutoka kwa JB Mpiana,” alisema mkali huyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya QS Muhonda, Joseph Muhonda, waratibu wa maonesho hayo, amesema kuwa ni matarajio yao wakazi wa Dar es Salaam, Arusha na Mwanza, watafurahia shoo hiyo kutoka kwa JB Mpiana na Mashujaa kutokana na maandalizi ya nguvu waliyofanya, akiwataka wakazi wa maeneo hayo, kujitokeza kwa wingi.
Alisema kuwa katoka onesho la JB Mpiana jijini Arusha, atatumbuiza katika ukumbi wa Triple A kuanzia saa tatu usiku, wakati Desemba Mosi atakuwa katika ukumbi wa Villa Park kuanzia saa tatu usiku.
“Maandalizi yote yapo sawa, kila kitu kimekamilika, tuliahidi JB Mpiana anakuja na kweli amekuja kama mlivyomuona,” alisema na kuongeza kuwa JB Mpiana atasindikizwa na wasanii wa Bongo Fleva kama H Baba, MB Doggy, Ney wa Mitego na wengineo.
No comments:
Post a Comment