Hector "Macho" Camacho |
Hector "Macho" Camacho |
Hector "Macho" Camacho |
SAN JUAN, Puerto Rico
MADAKTARI walitangaza jana Jumamosi kwamba bondia bingwa wa dunia wa zamani Hector "Macho" Camacho amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 50 baada ya mashine iliyokuwa ikisaidia uhai wake kuondolewa.
Kuondolewa kwa mashine hiyo kulifuatia ombi la mama yake mzazi, Maria Matias, baada ya kuambiwa na madaktari kwamba ubongo wa Camacho ulikuwa tayari umeshakufa. Mtoto wa kwanza wa bondia huyo, Hector Jr., alipinga kuondolewa kwa mashine hiyo, lakini mama huyo ndiye aliyekuwa na kauli ya mwisho. Hata hivyo, alitaka mashine hiyo iondolewe baada ya kuwasili kwa watoto wengine watatu wa bondia huyo kwa ajili ya kumuona kwa mara ya mwisho baba yao.
Camacho alishambuliwa kwa risasi za usoni na hakuzinduka tangu siku ya tukio. Mwenzake aliyekuwa naye garini alifariki katika eneo la tukio na polisi imesema hakuna mtu inayemshikilia na inashangazwa na tukio hilo ikisema haijui sababu.
Pamoja na mama yake, Camacho ameacha dada zake watatu, Raquel, Estrella na Ester; kaka yake Felix; na watoto wanne Hector Jr., Taylor, Christian na Justin.
Mama wa bondia hiyo, Maria Matias, aliwaambia waandishi wa habari nje ya hospitali ambayo Camacho alikuwa amelala akiwa hajitambui tangu alipopigwa risasi ya uso kwamba aliamua madaktari waitoe mashine iliyokuwa ikisaidia maisha yake kwa sababu mwanae alishakufa tangu siku tatu nyuma.
"Nilimpoteza mwanangu (Camacho) siku tatu zilizopita. Hivi sasa yuko hai kwa sababu ya mashine tu," mama Matias alisema juzi. "Mwanangu hayuko hai. Mwanangu yuko hai kwa ajili ya watu wanaompenda tu," aliongeza.
Mama wa bingwa huyo wa zamani ndiye aliyekuwa na kauli ya mwisho kwenye suala hilo, lakini mtoto wa kwanza wa bondia huyo, Hector Jr., alitaka kumuacha baba yake akiwa hai.
"Baba atapambana mpaka mwisho. Baba yangu ni bondia," mtoto huyo wa kiume alisema.
Madaktari walisema ubongo wa Camacho ulishakufa kutokana na risasi alizopigwa Jumanne usiku katika mji wa nyumbani kwao wa Bayamon. Lakini ndugu na marafiki waliliambia shirika la habari la Associated Press bado walikuwa wakipambana kama waondoe mashine hiyo ama waiache.
"Ni maamuzi magumu sana, maamuzi mazito sana," bondia wa zamani wa kulipwa Victor "Luvi" Callejas, rafiki wa muda mrefu wa Camacho, alisema katika mahojiano ya njia ya simu. "Jambo la mwisho kabisa ni kukataa tamaa na kupoteza matumaini. Kama hatujakata tamaa na tunayo matumaini, kwanini tusisubiri japo kidogo?"
Aida Camacho, mmoja wa shangazi za bondia huyo, alisema katika mahojiano kwamba familia ingeamua Ijumaa usiku kuhusu kuchangia viungo vilivyopungua.
Wakati ndugu na marafiki wakiendelea kusali kuomba miujiza, rambirambi ziliendelea kuwasilishwa kwenye familia ya Camacho na maandalizi ya msiba na mazishi yameanza.
Gavana Luis Fortuno aliita kuwa hilo ni pigo kubwa la ghafla. "'Macho' daima atakumbukwa kwa uanamichezo wake na upendo ndani na nje ya ulingo," alisema.
Mwingine aliyetuma salamu za rambirambi wakati Camacho akiwa bado anapumulia mashine alikuwa ni gavana aliyechaguliwa Alejandro Garcia Padilla, ambaye alimshinda Fortuno katika uchaguzi wa Novemba.
"Maisha ya Macho Camacho, kama ya magwiji wetu wengine wa michezo, yaliiunganisha nchi yetu," alisema. "Tulisherehekea mataji yake mitaani na tulimpigia makofi."
Camacho alipigwa risasi akiwa amekaa kwenye gari na rafikie, Adrian Mojica Moreno (49), ambaye aliuawa katika shambulio hilo. Msemaji wa Polisi, Alex Diaz alisema maofisa walikuta vipakti vidogo tisa ya cocaine katika mfuko wa rafikiye na kimfuko cha 10 kikiwa kimefunguliwa ndani ya gari.
Polisi waliripoti kuwa hakuna mtu aliyekamatwa na kwamba wapelelezi wanaendelea kuwahoji mashuhuda. Kapteni Rafael Rosa aliwaambia waandishi wa habari Ijumaa kuwa wanafuatilia dondoo kadhaa walizopata, lakini aliongeza kwamba mashuhuda wachache sana wametoa ushirikiano. Alikataa kusema kama Polisi imebaini watuhumiwa fulani.
Hector Camacho Jr. alisema matukio ya uhalifu yanayoiandama Puerto Rico, kisiwa cha Marekani chenye takriban watu milioni 4, yaliripotiwa kuwa 1,117 mwaka jana idadi ambayo ni rekodi.
"Vifo, jela, dawa za kulevya, mauaji," alisema. "Hivyo ndivyo ilivyo mitaa yetu hivi sasa."
Dada za Camacho walisema kuwa wangependa kuusafirisha mwili wa Camacho hadi New York na kwenda kumzika kule. Camacho alikulia mjini Harlem, na akapata jina la utani la "Harlem Heckler."
Alishinda mataji ya ubingwa wa dunia katika uzani wa super lightweight, lightweight na junior welterweight katika miaka ya 1980 na alipigana mapambano makubwa kama dhidi ya Felix Trinidad, Julio Cesar Chavez na Sugar Ray Leonard. Camacho alimpiga kwa KO Leonard mwaka 1997, na kuhitimisha ndoto za kurejea kwa bingwa huyo wa zamani. Camacho alikuwa na rekodi ya 79-6-3.
Camacho alipambana na matatizo mengi binafsi kama utumiaji wa dawa za kulevya, pombe na matatizo mengine maishani mwake. Alihukumiwa kifungo miaka 7 gerezani mwaka 2007 kutokana na kesi ya wizi, lakini jaji aliamua kukifanya kuwa kifungo cha nje na kuacha mwaka mmoja tu gerezani. Aliishia kutumikia wiki mbili gerezani, baada ya kukiuka masharti ya kifungo cha nje. Mkewe pia mara mbili alifungua mashitaka ya kupigwa kabla ya hawajatalikiana.
No comments:
Post a Comment