Sunday, November 25, 2012

KILIMANJARO STARS YAANZA KWA KISHINDO CHALENJI... BOCCO ATUPIA MBILI

Mshambuliaji wa timu ya Kilimajaro Stars, Simon Msuva akimfungisha tela beki wa timu ya taifa ya Sudan, Faris Abdallah wakati wa mechi yao ya Kundi B la michuano ya Kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Namboole mjini Kampala leo jioni.
Mashabiki wa timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) waliosafiri kutoka Bukoba hadi Uganda wakishangilia timu yao wakati wa mechi yao ya Kundi B la michuano ya Kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Namboole mjini Kampala leo jioni.

JOHN Bocco 'Adebayor' alifunga mara mbili na kusaidia kuipa Kilimanjaro Stars mwanzo mzuri wa michuano ya Kombe la Chalenji wakati timu hiyo ya Tanzania Bara ilipochapa Sudan kwa magoli 2-0 katika mechi ya Kundi B kwenye Uwanja wa Namboole nchini Uganda leo jioni.

Nyota huyo wa klabu ya Azam, aliyeibuka mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita, aliifungia Kili Stars goli la kuongoza katika dakika ya 14 kufuatia ushirikiano mzuri baina ya Mwinyi Kazimoto na Mrisho Ngassa aliyemsetia Bocco kufunga katika goli tupu baada ya kipa
Abd Elrahman Ali kutoka kwenda kujaribu kumzuia Ngassa.  

Bocco alifunga goli la pili katika dakika ya 28 kufuatia kazi nzuri tena ya Ngassa aliyekimbia na mpira kwa kasi na kupiga shuti ambalo lilikuwa likielekea wavuni lakini ili kuwa na uhakika, Bocco aliliongeza nguvu baada ya kumpa mwili beki aliyekuwa akikimbilia kwenda kujaribu kuokoa.

Kwa ushindi huo, Kili Stars ilianzia katika nafasi ya pili ya msimamo kutokana na pointi 3, sawa na vinara Burundi ambao walifungua mechi za kundi hilo kwa kuisambaratisha Somali kwa magoli 5-1. Magoli katika mechi hiyo yalifungwa na Chriss Nduwarugara na Selemani Ndikumana wa Burundi waliofunga mawili kila mmoja na moja la Yusuph Ndikumana. La Somalia lilifungwa na Mohammed Jabril kwa 'tuta' lililopigwa chini katikati ya lango likimuacha kipa akihama mahala hapo. 

Kilimanjaro Stars itacheza mechi yake ijayo Jumatano wakati itakapowakabili vinara Burundi saa 12:00 jioni katika mtihani mwingine mkubwa kwa kocha Mdenmark Kim Paulsen wa Kilimanjaro Stars. Mechi hiyo Jumatano itatanguliwa na mechi nyingine ya Kundi B baina ya timu ambazo hazina pointi, Somalia na Sudan saa 9:00 alasiri.


Wawakilishi wengine wa Tanzania, timu ya Zanzibar Heroes ya Zanzibar itacheza mechi ya ufunguzi wa Kundi C kesho dhidi ya Eritrea saa 10:00 jioni wakati Rwanda watawavaa Malawi saa 12:00 jioni.


Vikosi jana vilikuwa; Kilimanjaro Stars: Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Kelvin Yondani, Salum Aboubakar, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Simon Msuva na John Bocco 'Adebayor'.


Sudan: Abd Elrahman Ali, Moawia el Amin, Sami Abdallah, Faris Abdallah, Hamoda Bashir, Mohammed el Murtada, Sadam Abutalib, Mohammed Idris, Modathir Mohammed, Adam Sayer na Mohammed Osman. 

----------

No comments:

Post a Comment