Saturday, November 24, 2012

HATIMAYE YANGA WAINGIA MKATABA NA WACHINA WALIOJENGA UWANJA WA TAIFA ILI WAFYATUE BONGE LA UWANJA WA KISASA KWENYE MAKAO MAKUU YAO JANGWANI... UTAKUWA UKIINGIZA MASHABIKI 40,000... MKATABA WASAINIWA LEO KATI YA MWENYEKITI WA YANGA YUSUF MANJI NA MENEJA MKUU WA KAMPUNI YA KICHINA AITWAYE DAVID ZHANG... ULE WA SIMBA ULIOAHIDIWA NA RAGE KIMYAAA..!

Tunataka Yanga tuwe na uwanja wetu....! Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji.
Sehemu ya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam uliojengwa na kampuni ya Kichina ya Beijing Constructions Engineering.
Wakati uongozi wa Simba ukiendelea 'kumbwelambwela' kuhusiana na utekelezaji wa ahadi ya kujenga uwanja mkubwa wa kisasa utakaogharimu Sh. bilioni 74, wenzao wa Yanga walau wameanza kuonyesha dalili za kujikwamua kivitendo kwa kuingia mkataba leo na kampuni ya ujenzi ya kichina ya Beijing Constructions Engineering kujengewa uwanja wa kisasa utakaokuwa ukichukua watazamaji 40,000 pindi utakapokamilika.

Uwanja huo ni uleule wa Kaunda uliopo katika makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo kwenye makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani na wajenzi wake, kampuni ya Kichina ya Beijing, ndiyo walewale waliojenga Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Waliosaini mkataba huo mbele ya waandishi wa habari leo kwenye makao makuu ya jengo la Yanga ni Yussuf Mehboob Manji ambaye ni mwenyekiti wa mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) huku David Zhang ambaye ni Meneja Mkuu wa Beijing Construction Engineering akisaini kwa niaba ya kampuni yake kutoka China.

Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo, Manji alisema kwamba uongozi wake unayo furaha kubwa kwani hatua hiyo ni mwanzo wa harakati zao za kujikwamua kiuchumi.

Manji alisema vilevile kuwa hivi sasa wanafikiria kulijenga upya jengo lao lililopo katika Mtaa wa Mafia jijini Dar es Salaam ili lianze kuzalisha zaidi na kuwa sehemu ya vyanzo vyao vya mapato.

Wataalam wa kampuni iliyopewa tenda hiyo ya Beijing Costructions wataanza kazi yao Jumatatu kwa kutua na zana zao za kazi ya awali ya kuchukua vipimo kabla ya shughuli nzito ya ujenzi kamili kuanza Juni, 2013; lakini baada ya uongozi kupata idhini ya wanachama wakati wa mkutano mkuu wao utakaofanyika Desemba 8.

Kwa upande wake, Zhang alisema kuwa wamefurahi kupata 'dili' la kujenga uwanja wa Yanga na anaahidi kufanya kazi yao kwa ukamilifu wa hali ya juu kama walivyoujenga Uwnaja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Aidha, tofauti na uongozi wa watani zao Simba ambao hawakutaja chanzo cha fedha za kukamilisha mradi wa ujenzi wa uwanjao wao wa Sh. bilioni 74 na kudaiwa kuwa utashughulikiwa na wakandarasi kutoka Uturuki, Yanga waliweka wazi sula hilo kwa kusema kuwa wanatarajia kupata sehemu ya fedha kutoka kwa wanachama wa klabu yao na nyingine wanatarajia kupata kutoka katika mikopo watakayoomba benki. Uwanja wa Taifa ulijengwa na serikali kwa msaada wa serikali ya China kwa Sh. bilioni 56. Hata hivyo, haikuelezwa Yanga watahitaji kiasi gani cha fedha za mradi huo kwani itajulikana baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu..

Hadi sasa, uongozi wa Simba bado haujaeleza kiundani ni wapi wamefikia katika mpango wa ujenzi wa uwanja wao wa kisasa waliodai wataujenga eneo la Bunju jijini Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment