Thursday, October 4, 2012

HATMA YA UTATA UMRI WA LULU KUJULIKANA KESHO

Elizabeth Michael "Lulu"

MAHAKAMA ya Rufani inatarajia kuamua kesho kama Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Dar es Salaam isikilize maombi ya utata wa umri wa msanii wa Bongomuvie, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu (18), anayekabiliwa na shtaka la mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba 'The Great' (28).


Hatua hiyo imefikiwa baada ya Jopo la Majaji watatu likiongozwa na Mwenyekiti Jaji  January Msoffe, Bernard Luanda na Edward Rutakangwa ambao walihoji pande mbili kwanini suala hilo limefikishwa mahakamani hapo badala ya kuendelea na usikilizwaji wa awali katika Mahakama ya Kisutu.


Septemba 17, mwaka huu jopo hilo liliketi na kusikiliza hoja za kisheria zilizotolewa na pande zote mbili kabla ya kuliahirisha hadi kesho watakapotoa uamuzi huo.


Awali, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Faraja Nchimbi akisaidiana na Wakili wa Serikali Shadrack Kimaro, ulidai kuwa umeomba mapitio kwa sababu katika uamuzi uliotolewa na Jaji Dr. Fauz Twaib alikiri maombi ya utetezi hayakuwasilishwa mahakamani kihalali kwa mujibu wa sheria.


Alidai kuwa, Jaji Dk. Twaib alitakiwa kuyaondoa maombi hayo badala yake alikubali kuyasikiliza wakati alibaini kuwa hayako sahihi.


“Jaji Dk. Twaib alikosea kutoa tafsiri ya kifungu cha 44 (1) cha sheria ya mahakimu alipaswa kutoa maelekezo kwa Mahakama ya Kisutu kulingana na makosa aliyoyaona katika uamuzi wa Hakimu Mkazi Augustina Mmbando na siyo kuyasikiliza yeye mwenyewe… tumeamua kuomba mapitio ili yasikilizwe haraka badala ya kukata rufaa,” alidai Nchimbi.


Alifafanua kuwa msingi wa malalamiko yao mahakamani hapo ni kuhusu uamuzi uliotolewa na Jaji Dk. Twaib kwamba ulikuwa na dosari kwa kuzingatia bado hoja ya msingi ilikuwa pembeni.


Jaji Msofe aliuhoji upande wa utetezi kwanini shauri hilo limefika Mahakama Kuu Tanzania, wakati Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji na kwa sababu gani wasingesubiri shauri lianze kusikilizwa usikilizwaji wa awali katika mahakama kuu baada ya upelelezi kukamilika.


Akijibu hoja hizo, wakili wa utetezi Peter Kibatala alidai kuwa waliwasilisha maombi yao  kwa sababu ya kulinda maslahi ya mtoto (mshtakiwa).


Mbali na Kibatala wakili mwingine wa utetezi ni Kennedy Fungamtama ambao waliwasilisha maombi mahakama kuu wakidai kuwa ana umri wa miaka 17 na siyo miaka 18 kama ilivyoandikwa kwenye hati ya mashtaka.


Katika kesi hiyo, Lulu anadaiwa kuwa Aprili 7, mwaka huu Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alimuua Kanumba.


Aidha, kwa mujibu wa Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA), Lulu hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji lakini mara upelelezi wake utakapokamilika itahamishiwa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment