Thursday, September 6, 2012

TBL YAMWAGA VIFAA SIMBA, YANGA

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe (wa pili kushoto), akikabidhi vifaa vya michezo kwa Msemaji wa Klabu ya Yanga, Louis Sendeu (kushoto), ikiwa ni sehemu ya udhamini wa kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji hicho kwa Klabu za Simba na Yanga, katika hafla iliyofanyika kwenye Ofisi ya TFF, jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' na Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba. PICHA: JOHN BADI
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe (wa pili kushoto), akikabidhi vifaa vya michezo kwa Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' , ikiwa ni sehemu ya udhamini wa kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji hicho kwa Klabu za Simba na Yanga, katika hafla iliyofanyika kwenye Ofisi ya TFF, jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Msemaji wa Klabu ya Yanga, Louis Sendeu na Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba. PICHA: JOHN BADI

Msemaji wa Klabu ya Yanga, Louis Sendeu (kushoto) na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' (kulia) wakionyesha kwa waandishi wa habari baadhi ya vifaa vya michezo baada ya kukabidhiwa na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe (wa pili kushoto), ikiwa ni sehemu ya udhamini wa kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji hicho kwa Klabu za Simba na Yanga, katika hafla iliyofanyika kwenye Ofisi ya TFF, jijini Dar es Salaam jana. Wa (pili kulia) ni na Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba. PICHA: JOHN BADI

KLABU za Simba na Yanga jana zilipokea jezi na vifaa vingine mbalimbali vya michezo kutoka katika Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara  itakayoanza Septemba 15.

Akizungumza jana kabla ya kukabidhi vifaa hivyo, Meneja Mkuu wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, alisema kuwa vifaa hivyo ambavyo ni pamoja na jezi za kuchezea katika mechi za nyumbani na ugenini vina thamani ya Sh. milioni 68, ambapo kila timu imepata vifaa vya thamani ya Sh. milioni 34.


Kavishe alisema kuwa makabidhiano hayo ni sehemu ya makubaliano yaliyoainishwa kwenye mkataba walioingia ili kuhakikisha wanajiandaa vyema na mechi za ligi na mashindano ya kimataifa ambayo timu hizo mbili wanapata nafasi ya kushiriki.


Alisema kwamba udhamini wao katika klabu hizo kongwe unalenga kuendeleza soka la Tanzania kwa sababu wao pia hupata faida kutokana na timu hizo mbili kuwa na mashabiki wengi hapa nchini.


Alieleza kuwa vifaa hivyo ni kwa ajili ya mzunguko wa kwanza wa ligi na mwakani watatoa vifaa vingine ambavyo vitatumika kwenye duru la lala salama ya ligi hiyo.


Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu', alisema kuwa wanaishukuru TBL kwa kutimiza makubaliano yao na wanaahidi kwamba watafanya vizuri kwenye ligi hiyo na kutetea ubingwa wao.


Kaburu alisema kuwa Simba itatumia vifaa hivyo kikamilifu na kueleza kwamba imefanya maandalizi mazuri na iko tayari kuanza vyema msimu mpya wa 2012/ 2013.


Msemaji wa Yanga, Louis Sendeu, alisema jana kwamba watatumia vyema vifaa vyote hivyo na kuhakikisha wanafanya vizuri kama ilivyokuwa wakati wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) iliyofanyika nchini hivi karibuni.


Sendeu aliwataka pia wadhamini hao kuziangalia klabu nyingine za ligi hiyo ambazo zinasuasua katika kujiendesha kutokana na tatizo la fedha.


Naye Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Saad Kawemba, alisema jana kuwa wanaishukuru TBL kwa kuendelea kushiriki katika juhudi za kukuza mchezo wa soka nchini.


Kawemba alisema kwamba TBL kwao si wadhamini wala wafadhili bali ni washirika.


Mbali na kutoa vifaa, TBL pia hutoa motisha ya Sh. milioni 40 kwa timu inayobeba ubingwa kati ya hizo na pia hutoa Sh. milioni 25 kwa mshindi wa pili. Yanga waliambulia kapa msimu uliopita baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Bara.

No comments:

Post a Comment