Wednesday, September 5, 2012

TAZAMA DAUDI MWANGOSI WA CHANEL TEN ALIVYOZIKWA KIJIJINI KWAO, UJUMBE WALIOTOA MSIBANI DK. SLAA WA CHADEMA, WAZIRI PROF. MWANDOSYA WA CCM NA KAULI YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI DK. EMMANUEL NCHIMBI WAKATI AKITANGAZA TUME YA KUSAKA MAJIBU YA MASWALI SITA MUHIMU KUHUSIANA NA TUKIO LA KUUAWA MWANDISHI HUYO KWA KUPIGWA BOMU WAKATI AKIRIPOTI TUKIO LA SINTOFAHAMU YA POLISI NA CHADEMA IRINGA



Mjane wa marehemu, Itika Mwangosi (kulia) akilia wakati wa mazishi ya mumewe jana.

Mjane wa marehemu, Itika Mwangosi akilia kwa uchungu pembeni ya kaburi la mumewe, marehemu Daudi Mwangosi.

Mwili wa marehemu Mwangosi ukipelekwa makaburini
Inaelezwa kuwa huu ni mwili wa marehemu katika eneo la tukio baada ya kulipukiwa na bomu.
Askari wakiwa katika 'bifu' na marehemu Mwangosi (katikati) kabla ya kutokea kwa kifo chake. 

Mabaki ya mwili wa marehemu yakionekana chini katika eneo la tukio .
Wafuasi wa Chadema wakionekana na bendera zao katika siku ya tukio.
Gari la mbele ni la Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda... hapa ni katika siku ya tukio la kifo cha Mwangosi.
Askari wakiwa tayari kwa operesheni katika siku ya tukio la kuuawa kwa Mwangosi.
Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamuhanda. Hii ni katika siku ya tukio,
Mwangosi enzi za uhai wake.
ALIYEKUWA mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, amezikwa huku Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, akiunda tume ya kuchunguza mauaji yake, ambayo inahusisha wajumbe kutoka tasnia za sheria, habari, Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

 Mamia ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali jana walijitokeza kumzika Mwangosi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC). Marehemu aliyeuawa kwa kupigwa kwa bomu alizikwa majira ya saa 7.30 mchana kijijini kwake Busoka wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.

Mwangosi aliuawa Jumapili iliyopita katika kijijini cha Nyololo, wilayani Mufindi, mkoani Iringa katika tukio ambalo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walikuwa wakifungua tawi la chama chao, huku jeshi la Polisi likitumia nguvu kubwa yakiwemo mabomu ya machozi kuzuia uzinduzi wa tawi hilo.

Mamia ya wakazi wa kijiji hicho, wanasiasa wa vyama vya CCM na Chadema na waandishi wa habari kutoka mikoa ya Iringa na Mbeya walishiriki katika mazishi hayo.

Mwakilishi wa serikali katika mazishi hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais asiye na Wizara Maalum, Prof. Mark Mwandosya, akitoa salamu za rambimbambi katika msiba huo, alisema atabeba jukumu la kuwasomesha watoto wengine wa marehemu huyo huku akiahidi kufuatilia ahadi za watu wengine katika kuisaidia familia ya Mwangosi kwa kuwa ni ndugu yake na jirani.

“Nitahakikisha familia hiyo inaishi maisha kama ambavyo agelikuwepo baba yao kwa kuhakikisha kila mtoto wa familia hiyo anasoma kwa kila hatua kwa kuzingatia kuwa hao ni sehemu ya familia yangu,” alisema Mwandosya, ambaye pia ni Mbunge wa Rungwe Mashariki (CCM).

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema watabeba jukumu la kumsomesha mtoto wa kwanza wa Mwangosi aitwae Nehemiah, ambaye kwa sasa yupo kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Malangali iliyopo Mufindi, mkoani Iringa.

“Mtoto huyu alifika na kutaka kujua sababu za kifo cha baba yake kwa uchungu huku machozi yakimtoka, nimewasiliana na mdau wangu na kuahidi kubeba kujumu la kumsomesha na pia naahidi kufuatilia ahadi hiyo kwa kipindi chote cha masomo yake,” alisema Dk. Slaa.

Katibu Msaidizi wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Iringa (IPC), Francis Godwin, aliwatahadharisha wanasiasa kwamba Mwangosi atazikwa kama mwandishi wa habari japokuwa aliuawa katika tukio lililohusisha shughuli za kisiasa.

IPC walitoa kwa familia ya marehemu Sh. 700,550 kama rambirambi huku Klabu ya Waandishi mkoani Mbeya (MPC) nayo ikitoa kiasia kama hicho.

Wengine waliotoa rambirambi ni mlezi wa IPC, Salim Asas aliyetoa Sh. milioni moja, Taasisi ya Habari ya Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (Misa-Tan) Sh. 500,000 na Channel Ten Sh. 700,000. Wengine ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa (Chadema), Chiku Abwao Sh 100,000.

 Mazishi ya Mwangosi yalitawaliwa na vilio na simanzi kutoka kwa ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wengine waliohudhuria. Hata hivyo, Jeshi la Polisi halikuwa na mwakilishi katika mazishi hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam jana wakati wa kutangaza tume hiyo, Waziri Nchimbi alisema nia ni kupata matokeo yasiyoegemea upande wowote kwa kuwa tume iliyoundwa ni huru.
Alisema itaongozwa na Jaji mstaafu Stephen Ihema, huku wajumbe wakiwa ni Theophil Makunga kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ambaye pia ni Mhariri Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications; Ofisa Mipango wa Baraza la Habari Nchini (MCT), Pili Mtambalike; mtaalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Wema Wapo na Naibu Kamishna wa Polisi, Isaya Mngulu.

Tume hiyo imepewa hadidu za rejea sita na itafanyakazi kwa siku 30 kuanzia leo.

Hadidu hizo ni kuchunguza chanzo cha kifo cha Mwangosi, kama kuna uhasama kati ya waandishi wa Iringa na Polisi, kama kuna orodha ya waandishi watatu waliopangwa kushughulikiwa na polisi mkoani humo, kama kuna taratibu za kukata rufaa ya vyama vya siasa dhidi ya polisi pindi mikutano yao inapozuiwa, je, kuna tatizo la mahusiano kati ya polisi na vyama vya siasa kwa ujumla wake na kama ukubwa wa nguvu zilizotumika katika tukio la Iringa ni sahihi.

Alisema kuna maneno mengi yanayozungumzwa kuhusu kuuawa kwa mwandishi huyo, hivyo matokeo ya uchunguzi wa tume yataweka wazi uhalisia wa mauaji hayo.

Alipohojiwa kuhusu kampeni za uchaguzi mdogo zinazoendelea katika Jimbo la Bububu pamoja na maandamano ya wananchama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaorudisha fomu, Nchimbi alisema kinachofanyika uko kinaratibiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), hivyo yenyewe inaweza kuwa na majibu mazuri kuhusu swali hilo.

Kuhusu mikutano ya CCM na maandamano ya wagombea, alisema zuio la msajili wa vyama vya siasa linavihusu vyama vyote na hata alipopata taarifa ya mikutano hiyo aliwasiliana na viongozi wa CCM ambao walimjibu kwamba wanafanya mikutano ya ndani.

“Hakuna upendeleo wowote kwa vyama, maandamano na mikutano yote ya hadhara imezuiwa, lakini ieleweke kwamba hatujazuia mikutano ya ndani ya vyama,” alisema.

Alisema anasikitishwa na mauaji ya raia au uonevu wowote wa raia na ni mambo ambayo hawezi kamwe kuyavumilia wala kumvumilia askari anayenyanyasa raia.

Alisema atashughulikia na askari wachache wanaolipaka matope Jeshi la Polisi na atawawajibisha wote watakaobainika kunyanyasa raia.

Alipoulizwa kama atakuwa tayari kujiuzulu wadhifa wake ikiwa tume itabaini Polisi ndio waliomwua Mwangosi, alisema: “Nikiondoka hapa mtanikumbuka sana ninyi, mimi nitawafanyia mambo makubwa, ninachoomba tusubiri tume imalize muda wake.”

Alisema anafanya kazi bila kupuuza malalamiko ya raia na kwamba ni muumini wa utawala wa sheria, hivyo anasimamia sheria katika utendaji wake wa kila siku.

Waandishi walimkumbusha tume za nyuma zilivyochelewesha matokeo ya uchunguzi ambayo pia hayakuchukuliwa hatua madhubuti kwa kuwa yamekuwa yakilisafisha Jeshi la Polisi, alisema matokeo ya tume yake yatafanyiwa kazi na ikibainika askari wamehusika watawajibishwa.

 Alisema hadi sasa hakuna askari anayeshikiliwa wala ambaye amesimamishwa kupisha uchunguzi kwa kuwa wanaowachunguza ni askari wenye vyeo vikubwa ambao hawawezi kuingiliwa katika uchunguzi.

Alisema baada ya kuuawa kwa kijana mkoani Morogoro wiki mbili zilizopita, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema, alikutana na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Slaa na kuzungumza naye kwa kirefu na kumwomba asitishe kwa muda mikutano ya hadhara; Dk. Slaa akakubali, lakini katika hali ya kushangaza mikutano hiyo iliendelea.

RPC IRINGA, CHAGONJA WASIMAMISHWE
Chadema kimetaka Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo, Paul Chagonja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, wasimamishwe kazi ili kupisha uchunguzi wa kifo hicho.

 Chadema pia imetaka askari saba wanaoonekana kwenye picha wakimpa kipigo marehemu Mwangosi wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria mara moja kwani hakuna haja ya kufanya uchunguzi wakati wanaonekana wakimfanyia unyama mwandishi huyo.

Tamko hilo la Chadema lilitolewa na Mkurugenzi wake wa Habari na Uenezi, John Mnyika, alipozungumza na waandishi wa habari, makao makuu ya chama hicho jana jijini Dar es Salaam.

 Alisema iwapo mambo hayo hayatatekelezwa, uchunguzi utakaofanyika itakuwa ni upotevu tu wa pesa za Watanzania.

“Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) licha ya kwenda Iringa, cha kushangaza bado askari wanaoonekana kuhusika katika mauaji ya mwandishi huyo hawajachukuliwa hatua ya kukamatwa. Wananchi wataielewaje serikali?” alihoji Mnyika.

Alisema Kamishna Chagonja tangu mwanzo wa tukio hilo amekuwa akitoa maelezo ya uongo yanayopotosha umma, ambayo pia yanatofautiana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, hali inayotia shaka kama uchunguzi wa tukio hilo utakuwa wa haki.

Mnyika alisema imeshafahamika kuwa marehemu aliuawa kwa kutupiwa bomu, uchunguzi unatakiwa uanzie ni ofisa gani wa Jeshi la Polisi alitoa agizo hilo na kusababisha mauaji hayo ya kinyama kwa mwandishi huyo.

Alisema kutokana na mfululizo wa mauaji ya vijana yanayofanywa na polisi dhidi ya raia wakati wa mikutano ya kisiasa, Chadema imekuwa ikipata ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms) kutoka kwa wananchi mbalimbali, ambao wanatoa mapendekezo ya nini kufanywe na chama hicho katika kukabiliana na tatizo hilo, ambalo limeamsha hasira zao.

Mnyika alisema miongoni mwa mapendekezo yanayotolewa na Watanzania ni pamoja na kuitaka Chadema ichukue hatua kwa kushitaki katika mahakama za ndani au za kimataifa ili kuhakikisha haki inapatikana.
Mnyika alisema kama polisi wanashikilia msimamo wa kwamba, Chadema walivunja sheria kwa kufanya mkutano wakati serikali imepiga marufuku mikutano ya kisiasa isifanyike hadi sensa imalizike, basi waanze kumchukulia hatua Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal.

Chanzo: Gazeti la NIPASHE (Jumatano Septemba 5, 2012)


No comments:

Post a Comment