Mabingwa wa Dunia, Hispania hawakuanza kampeni zao hadi Jumanne, lakini ukiacha Waitalia, walioshikiliwa kwa sare ya 2-2 katika Kundi B ugenini Bulgaria, hapakuwa na matatizo makubwa kwa mataifa makubwa ya Ulaya.
England walishinda mechi yao ya ufunguzi wa Kundi H kwa mabao 5-0 ugenini Moldova, wakati Ujerumani walipata ushindi wa 3-0 katika Kundi C dhidi ya Visiwa vya Faroe.
Goli la kipindi cha kwanza la Abou Diaby liliwapa Ufaransa mwanzo mzuri wa ushindi wa 1-0 katika Kundi I dhidi ya Finland mjini Helsinki, wakati Uholanzi waliwafunga Uturuki 2-0 mjini Amsterdam katika mechi ya Kundi D kupitia mabao ya Robin van Persie na Luciano Narsingh, ambaye alifunga goli la pili katika dakika za lala-salama.
Italia, ambao wamekuwa mabingwa wa dunia mara nne, walikuwa na mwanzo mgumu mjini Sofia ambako walishikiliwa kwa sare ya 2-2 dhidi ya Bulgaria baada ya Pablo Osvaldo kuwafungia magoli yao yote mawili na kuwaweka mbele 2-1 kufuatia ya kutangulia kufungwa.
Georgi Milanov aliwasawazishia wenyeji zikiwa zimebaki dakika 24 mechi kumalizika na Italia waliojaza vijana, hawakuweza kupata goli la ushindi.
Waitalia wawili ambao walikuwa na usiku mzuri kuliko timu yao ya taifa walikuwa ni Fabio Capello na Giovanni Trapattoni, makocha wa timu za taifa za Urusi na Ireland.
Jaribio la Ireland kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2002 lilianza na ushindi wa aina yake kupitia magoli mawili ya dakika mbili za mwisho wa mechi kutoka kwa Robbie Keane, ambaye alifunga penalti, na kuunganisha juu kwa juu krosi ya Kevin Doyle na kukipa kikosi cha Trapattoni ushindi wa 2-1 nchini Kazakhstan katika Kundi C.
Urusi ya Capello ilianza kwa ushindi pia, kupitia magoli ya Viktor Faizulin na Roman Shirokov, ambaye alifunga penalti, na kuwapa ushindi wa 2-0 dhidi ya Ireland Kaskazini mjini Moscow.
Mechi iliyokuwa na "mvua ya mabao" ilikuwa ni ya Bosnia, ambao walianza kampeni yao ya kufuzu kwa mara ya kwanza kwa kuwasambaratisha Liechtenstein 8-1 mjini Vaduz katika Kundi G.
Edin Dzeko, ambaye alifunga 'hat-trick', amekuwa mchezaji aliyeifungia timu hiyo ya taifa magoli mengi zaidi katika historia yao akiwa amefunga magoli 25.
MBILI ZA LAMPARD
England walifunga magoli mengi dhidi ya Moldova huku Frank Lampard akifunga mara mbili katika dakika 29 za kwanza, la kwanza katika dakika ya 3 kwa kutumia penalti ya 100 ya England katika historia, wakati alipofikisha jumla ya magoli yake kwa timu yake ya taifa ya England kuwa 25.
Jermain Defoe aliyecheza mechi yake ya 50 kwa England alifunga kwa moja ya mashuti yake maarufu katika dakika ya 32 huku James Milner na Leighton Baines wakifunga magoli yao ya kwanza kwa timu yao ya taifa.
Mesut Ozil alifunga mara mbili, akipachika mabao hayo yote katika kipindi cha pili kufuatia goli la kwanza la Mario Goetze katika kipindi cha kwanza wakati Ujerumani ilipoifunga Faroes 3-0 mjini Hanover.
Uholanzi pia ilizoa pointi zote tatu baada ya mwanzo mbaya wakati Uturuki walipokaribia kufunga goli katika dakika ya kwanza kupitia kwa Omer Toprak lakini Van Persie na baadaye Narsingh walifunga na kuipa timu yao ushindi wa 2-0.
Ureno hawakuwa na mechi rahisi kabla ya kushinda 2-1 ugenini Luxembourg baada ya wenyeji ambao hawapewi nafasi kupata uongozi wa kustukiza kupitia kwa mzaliwa wa Ureno, Daniel da Mota katika dakika ya 13.
Cristiano Ronaldo, ambaye alitawala vichwa vya habari baada ya kutoshangilia magoli yake mawili kwa Real Madrid wikiendi iliyopita na kuwaambia waandishi wa habari kwamba hana furaha, alisawazisha dakika 15 baadaye.
Alishangilia goli hilo la kusawazisha kwa kupiga ngumi hewani.
Wageni waliendelea kuwaandama wenyeji na kupata goli la kuongoza walilostahili kwa shuti lililopigwa kiufundi na Helder Postiga katika dakika ya 54.
Ubelgiji, ambao kikosi chao kinachoinukia kinaundwa na wachezaji wenye vipaji wanaotamba katika Ligi Kuu ya England, walianza vyema kampeni zao za kwenda kwenye fainali Brazil kwa ushindi wa 2-0 ugenini Wales ambapo nahodha wa Manchester City, Vincent Kompany na beki mpya wa Tottenham Hotspur, Jan Vertonghen walifunga magoli ya ushindi.
Kulikuwa na upinzani mkali, kadi nyekundu mbili na kulipuliwa kwa mafataki mjini Podgorica katika mechi baina Montenegro na Poland, ambazo ziko kundi moja na England, zilizotoka sare ya 2-2.
Jumla ya mechi 22 za kufuzu zilichezwa jana na mbili zaidi zitapigwa leo huku raundi ya pili ya kuwania kufuzu kwa kanda ya Ulaya zikichezwa Jumanne, ambapo itawashuhudia mabingwa watetezi wa dunia Hispania wakianza mjini Tbilisi dhidi ya Georgia ambao wataingia uwanjani wakijiamini kwa ushindi wao wa jana wa 1-0 dhidi ya Belarus.
No comments:
Post a Comment