Thursday, September 6, 2012

MUIGIZAJI STEVE NYERERE AJITOSA KWENYE SIASA

Steven Mengele a.k.a Steve Nyerere

MSANII nyota wa filamu nchini Steven Mengele maarufu kama Steve Nyerere juzi alirudisha fomu na kufanyiwa usaili katika Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni ambapo anawania nafasi ya kuingia katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC).

Akizungumza baada ya kufanyiwa usaili, Steve Nyerere alisema kwamba yuko tayari kuwatumikia vijana na wasanii kwa ujumla ikiwa ni njia mojawapo ya kutetea haki za wasanii wote nchini.

“Huu ni mwanzo tu na na nimejitosa katika siasa ili niweze kuungana na wanachama wa chama ninachokipenda cha CCM na kuwawakilisha wasanii na vijana kwa ujumla,” alisema Steve.

Aliongeza kuwa amethubutu kuingia katika siasa siyo kwa kushurutishwa bali amejikuta wito ukimtuma afanye hivyo na kusema kwamba amepata hamasa kubwa kwa wasanii wenzake ambao wametangulia na kuwa wajumbe wa NEC kama Khadija Kopa na John Komba.

Aidha, msanii huyo amepata baraka zote kutoka kwa Shirikisho la Filamu Nchini (TAFF) na endapo atateuliwa, anatarajiwa kuwa mwakilishi wa kwanza wa wasanii wa filamu nchini kuingia katika vikao hivyo vikubwa vya chama hicho.

Wakati huohuo, Steve Nyerere alisema kuwa endapo atashindwa kupata nafasi ya ujumbe wa NEC hatakata tamaa na atajipanga na kuangalia alipokosea na si kukihama chama chake kwa kuwa ana mapenzi mema na chama hicho.

Nyerere kwa sasa anatamba na filamu ya ‘Mwalimu Nyerere,’ aliyoizindua hivi karibuni katika kituo cha watoto yatima cha Maunga Center.

No comments:

Post a Comment