Tuesday, September 11, 2012

MNYAMA ABEBA NGAO KIKAMANDA... AZAM YAFA 3-2 LICHA YA KUANZA KWA KUONGOZA 2-0

Straika wa Simba, Mghana Daniel Akuffor (wa pili kushoto) akijaribu kumpita beki wa Azam, Aggrey Morris (aliyelala chini kuokoa) huku kipa Deogratius Munishi 'Dida' (kulia) akiwa tayari kusaidia wakati wa mechi yao ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo. Simba ilishinda 3-2 na kutwaa ngao hiyo kwa mara ya pili mfululizo. 

LICHA ya kuanza kwa kutanguliwa 2-0, Simba ilizinduka na kushinda 3-2 dhidi ya Azam katika mechi yao ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.


Azam waliona kama wangerudia mafanikio yao ya Kombe la Kagame walipoitoa Simba katika robo fainali kwa kuifunga magoli 3-1, wakati walipoongoza kwa magoli 2-0 katika dakika 35 leo kupitia kwa John Bocco na Kipre Tchetche.


John Bocco, ambaye aliwafunga Simba 'hat-trick' katika Kombe la Kagame, alitimiza magoli manne dhidi ya Simba katika mechi mbili alizokumbana nao wakati alipomzidi ujanja beki wa Nasoro Said 'Chollo' na kumfunga kipa Juma Kaseja katika dakika ya pili kabla ya mchezaji wa Ivory Coast, Tchetche, kuifungia Azam la bao pili akitumia pasi ya Bocco katika dakika ya 35.


Hata hivyo, Simba ilizinduka kupitia kwa Mghana Daniel Akuffor aliyefunga penalti iliyotolewa na refa Martin Saanya wa Morogoro baada ya beki Aggrey Morris kushika mpira ndani ya boksi dakika moja kabla ya mapumziko.


Mfumo wa 'kupaki basi' wa Azam huku mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi akikimbizwa na wachezaji watatu-watatu, uliwagharimu "wana-lambalamba" na kujikuta wakikaribisha mashambulizi mfululizo katika kipindi cha pili.


Simba ilipata goli la pili katika dakika ya 68 kupitia kwa Okwi, ambaye kukosekana kwake katika Kombe la Kagame kuliacha pengo la wazi katika kikosi cha kocha Mserbia Milovan Cirkovic.


Goli hilo lilionekana kuwachanganya Azam, ambao katika dimba la katikati hawakuweza kumtumia tangu mapema kiungo wao Salum Abubakar 'Sure Boy' ambaye ndio kwanza amerejea kutoka kuwa majeruhi.


Na Simba wakatumia udhaifu uliopo kupata goli la tatu kwa shuti la umbali wa takribani mita 30 kutoka kwa kiungo Mwinyi Kazimoto na kuwafanya mashabiki wa klabu hiyo ya Msimbazi walipuke kwa shangwe kubwa.


Ilikuwa ni Ngao ya Jamii ya pili mfululizo kwa Simba baada ya mwaka jana kuifunga Yanga 2-0 katika mechi hiyo maalum ya kufungua msimu wa ligi kuu ya Bara inayowahusisha mabingwa watetezi na washindi wa pili.


Kilikuwa ni kisasi kitamu dhidi ya timu hiyo iliyowafunga 3-1 kupitia mabao matatu yaliyofungwa na John Bocco katika Kombe la Kagame, licha ya kwamba Simba B iliwafunga wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Azam katika mechi ya Kombe la Urafiki.


Huku ikiwaanzisha kwa mara ya kwanza nyota wao wapya, Mrisho Ngassa aliye kwa mkopo na Ramadhani Chombo 'Redondo' aliyesajiliwa jumla dhidi ya klabu yao ya zamani, Simba ilidhihirisha makali yake inapokuwa na Okwi kikosini na kuwa tofauti na iliyolala 3-0 dhidi ya Sofapaka ya Kenya Alhamisi Septemba 6 katika mechi yao ya mwisho ya kujiandaa na pambano la leo.


Cirkovc aliwasifu wachezaji wake kwa kupambana kishujaa na kwa sababu mechi ilikuwa ngumu sana na akasisitiza kwamba wanafunga ukurasa huo na wako tayari kwa ligi kuu inayoanza Jumamosi.


Kocha wa Azam, Boris Bonjak, alilalamikia maamuzi akisema kwamba refa Saanya aliwapendelea Simba.


Vikosi vilikuwa; Simba: Juma Kaseja, Nasoro Said 'Cholo', Amir Maftah, Shomari Kapombe, Pascal Ochieng/ Juma Nyosso (dk.73), Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa, Ramadhani Chombo 'Redondo'/ Amri Kiemba (dk.69), Haruna Moshi 'Boban', Daniel Akuffor/ Abdallah Juma (dk.64) na Emmanuel Okwi.


Azam: Deogratius Munishi 'Dida', Erasto Nyoni, Ibrahim Shikanda, Aggrey Morris, Said Moras, Abdulhalim Homoud, Ibrahim Mwaipopo/ Salum Aboubakar 'Sure Boy' (dk.60), Himid Mao, Kipre Tchetche/ Zahor Pazi (dk.82), John Bocco 'Adebayor' na Abdi Kassim 'Babi'.  

No comments:

Post a Comment