Monday, September 10, 2012

MAKAMU WA RAIS IRAQ AHUKUMIWA KIFO

Makamu wa rais wa Iraq, Tariq al-Hashemi

MAHAKAMA nchini Iraq imepitisha hukumu ya kifo kwa makamu wa rais, Tariq al-Hashemi, baada ya kumkuta na hatia kwa kuongoza makundi ya kuuwa watu, yaliyowalenga Washia na askari wa usalama.

Makamo wa rais, wa madhehebu ya Sunni, hakuweko mahakamani wakati wa hukumu hiyo kwani alishaikimbia Iraq awali mwaka huu, akiwa sasa anaishi Uturuki.

Kesi hiyo imezusha msukosuko wa kisiasa katika serikali ya Iraq, iliyogawa madaraka kati ya Wa-Sunni, wa-Shia na WaKurd.

Bwana al-Hashemi amemshutumu Waziri Mkuu Nuri al-Maliki ambaye ni M-Shia, kuwa anawasaka wapinzani wake wa kisiasa wa madhehebu ya Sunni, lakini serikali inasisitiza kuwa kesi hiyo inafuata misingi ya sheria tu.

Hukumu hii ya mahakama imekuja huku watu wasiopungua 45 wakiwa wameuawa katika mfululizo wa mashambulizi 24 nchini Iraq. Siku ya Jumapili mashambulizi kadhaa yalishuhudiwa katika maeneo ya Tuz Khurmatu, Baquba, Basra na Samarra.

Wanajeshi 11 waliuawa kaskazini mwa Baghdad, huku katika mji wa Amara watu 14 wakiuawa na wengine 60 kujeruhiwa katika mashambulio mawili ya mabomu ya kutegwa katika gari.

Maafisa polisi saba pia waliuawa kwa bomu katika mji wa kaskazini wa Kirkuk, wakati wanajeshi kumi nao wakiuawa katika kambi ya jeshi ya Dujail kaskazini mwa Baghdad. Na katika eneo la Nasiriya kusini kulitokea mlipuko wa bomu nje ya ubalozi wa Ufaransa ulioua mtu mmoja huku serikali ya Ufaransa ikilaani shambulio hilo.

Hashimu alikuwa ni mwanasiasa wa juu sana aliyeheshimika kutoka dhehemu la Sunni katika serikali yenye Wa-Shia wengi hadi alipofunguliwa mashitaka mwezi December mwaka 2011 wakati alipotoroka nchini humo.

Wanasiasa wengine wa Ki-Sunni walimkataa waziri mkuu wa Ki-Shia Nouri al-Maliki aliyetoa amri ya kukamatwa kwa Bwana Hashemi, wakimuita kama dikteta na kumshutumu kwa kuendeleza chokochoko zinazoweza kuiingiza nchi hiyo katika vita vya kikabila kwa mara nyingine.

Waandishi wa habari wanasema muungano wa serikali kati ya Wa-Sunni, Wa-Shia na wale wa makabila mengine inaonkena kuwa hatarini tokea wakati huo.

Wapiganaji wa Ki-Sunni wanaohusishwa na kundi la kigaidi la al-Qaeda wamekuwa wakishutumiwa kwa vurugu za hivi karibuni nchini Iraq.

UHASAMA WA KIKABILA
Serikali ya Iraq ilitoa amri ya kukamatwa wa Bwana Hashemi mnamo tarehe 19 mwezi Desemba mwaka 2011, siku moja baada ya vikosi vya Marekani kuondoka nchini humo.

Alikimbilia kwanza katika eneo lenye Wa-kurdi wengi kaskazini mwa nchi, na baada ya hapo alikimbilia nchini Qatar na hatimaye nchini Uturuki.

Waendesha mashitaka wamesema Hashemi alihusika na mauaji ya watu 150. Wakati wa kesi hiyo iliyoendeshwa pasipo yeye kuhudhuria mjini Baghdad, walinzi wake wa zamani walisema kuwa Bwana Hashemi aliamuru mauaji hayo.

Hashemi mwenyewe anasema mashitaka hayo dhidi yake yameundwa kisiasa na kumshutumu Waziri Mkuu Maliki kwa kuendekeza ukabila.

Siku ya Jumapili mahakama nchini Iraq ilimkuta Hashemi na kijana mkwe wake kuwa na hatia ya mashitaka mawili ya mauaji na kumuhukumu adhabu ya kifo kwa kunyongwa. Jaji alitupilia mbali shitaka la tatu kwa kukosekana kwa ushahidi.

Ingawaje ghasia zimepungua tangu mwaka 2006 na 2007, mashambulizi yameongezeka tena baada ya vikosi vya Marekani kuondoka nchini humo mwishoni mwa mwaka jana, huku uhasama wa kisiasa na kikabila ukizidi kuongezeka.

Serikali ya Iraq imekuwa ikiathiriwa na mgawanyiko kati ya makundi ya kisiasa ya Sunni, Shia na Kurdi.

Serikali hiyo imesema mwezi Julai mwaka huu ulikuwa ni wa machafuko makubwa zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha karibu miaka miwili huku watu 325 wakiwa wameuawa.

Kiongozi wa zamani wa Iraq Saddam Hussein alikuwa M-Sunni na Wa-Sunni wengi wanaamini kuwa wamekuwa wakionewa na Wa-Shia waliojipatia umaarufu tokea uvamizi wa Marekani nchini humo.

Wa-Suni wamekuwa wakimshutumu Bwana Maliki kwa kuendesha mfumo wa utawala wa kibabe katika serikali yake.


CHANZO: BBC/Swahili

No comments:

Post a Comment