Robin van Persie |
LONDON, Uingereza
ARSENAL wameafiki 'dili' la kumuuza nahodha wao Robin van Persie kwa Manchester United, klabu hizo mbili pinzani za Ligi Kuu ya England ziliandika kwenye tovuti zao jana Jumatano.
Mshambuliaji huyo Mholanzi, ambaye alishinda kura ya mchezaji bora wa msimu uliopita, atasafiri leo kwenda Manchester kujadili malipo binafsi na kufanya vipimo vya afya kabla ya kutua rasmi Old Trafford.
Hamna maafikiano ya fedha yaliyotajwa na klabu hizo. Lakini vyombo vya habari vimeripoti kwamba Man United watalipa paundi milioni 24 kwa ajili ya Van Persie ambaye anajiandaa kusaini mkataba wa miaka minne na klabu hiyo.
Mdunguaji huyo mwenye umri wa miaka 29, ambaye pia amewavutia mabingwa wa Ligi Kuu ya England, Manchester City na Juventus, alisema mwezi uliopita kwamba hataongeza mkataba wake na Arsenal. Alikuwa amebakiwa na mwaka mmoja katika mkataba wake baada ya miaka minane na klabu hiyo ya London.
Van Persie alifunga magoili 37 msimu uliopita wakati Arsenal ilipomaliza ya tatu katika ligi na kufikia hatua ya 16-Bora ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya. Lakini klabu hiyo haijatwaa taji lolote tangu tangu mwaka 2005 ilipobeba Kombe la FA baada ya kuifunga Man United katika fainali.
Klabuni Old Trafford Van Persie anatarajiwa kuwa pacha wa mshambuliaji wa timu ya taifa ya England, Wayne Rooney wakati timu ya Alex Ferguson ikijaribu kurejesha taji kutoka kwa mahasimu wao wa mji mmoja Man City. Man United imesajkili mchezaji mmoja tu mkubwa tangu mwisho wa msimu uliopita, kiungo Mjapan Shinji Kagawa aliyejiunga akitokea kwa mabingwa wa Ujerumani, Borussia Dortmund.
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger alidhamiria kutorejea mwanzo mbaya kama wa msimu uliopita wakati uvumi wa kuhama kwa nahodha Cesc Fabregas na kiungo mwenzake Samir Nasri ulipoiyumbisha timu.
Fabregas alihamia Barcelona katikati ya Agosti na Nasri akauzwa kwa Manchester City siku tisa baadaye. Kabla ya mwisho wa mwezi huo Arsenal ilikumbana na kipigo cha "mbwa-mwizi" cha 8-2 dhidi ya Man United kwenye Uwanja wa Old Trafford.
No comments:
Post a Comment