Jose Mourinho |
NEW YORK, Marekani
JOSE Mourinho anaamini kuwa makali ya
klabu yake ya Real Madrid kuelekea ubingwa wa msimu uliomalizika wa La Liga,
Ligi Kuu ya Hispania 2011-12 yatabaki kuwa historia isiyovunjwa milele na klabu
yoyote ile, wakiwamo wao wenyewe.
"Kwanza kabisa, sidhani kama kuna
bingwa atakayefikisha tena pointi 100," Mourinho alisema katika mkutano na
waandishi wa habari baada ya timu yake kuishindilia AC Milan mabao 5-1 katika
mechi yao ya kirafiki ya maandalizi ya msimu jana jijini New York jana.
"Sidhani pia kama kuna bingwa atakayefunga
magoli 120. Nadhani hizi ni takwimu zitakazodumu katika historia kwa muda mrefu
sana."
Akizungumzia vita mpya kati ya Real
Madrid na Barcelona kuwania taji la La Liga msimu ujao, kocha huyo Mreno
alionekana kutambua kuwa mahasimu wao watakuwa wakali kama mbogo kutaka kutwaa
ubingwa huo.
"Kila mmoja anajua kwamba
kutakuwa na mchuano mkali sana, kwa mtazamo wangu, ni mchuano wa timu mbili zilizo
bora zaidi duniani," kocha huyo wa zamani wa Chelsea alisema.
"Kwa sababu katika msimu uliopita
tulikuwa na pointi nyingi sana na Barcelona walipata pointi nyingi pia, watu pengine
wanaweza kudhania kwamba ligi (La Liga) sio ngumu sana."
Lakini Mourinho aliongeza kwamba watu
ni lazima wafikirie zaidi ya timu hizo katika Ligi Kuu ya Hispania, akikumbushia
kwamba fainali ya Ligi ya Europa ilizikutanisha timu mbili za Hispania.
"Nakumbuka kwamba fainali ya Europa
ilikuwa ni kati ya Atletico Madrid na Atheltic Bilbao. Ligi hii (La Liga) ni ngumu,
ngumu sana," alisema.
No comments:
Post a Comment