Thursday, August 16, 2012
MAZOEZI MAKALI YAWAANGUSHA WACHEZAJI YANGA, KOCHA SAINTFIET APINGA TEGETE KUPELEKWA TOTO KWA MKOPO
Na Sanula Athanas
MABINGWA mara tano wa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga, leo waliendelea na kujifua kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola jijini Dar es Salaam kujiweka sawa kwa ajili ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu ujao huku baadhi ya wachezaji wao wakianguka kutokana na mazoezi makali ya kocha Tom Saintfiet.
STRAIKA ilishuhudia baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo ya Jangwani wakiishiwa nguvu na kuanguka uwanjani hapo kutokana na mazoezi magumu ya kukimbia na kupiga pasi huku wakikimbia yaliyokuwa yakitolewa na kocha huyo raia wa Ubelgiji.
Baada ya kutoa huduma kwa Shamte Ally, aliyeishiwa nguvu na kuanguka, daktari wa timu hiyo, Juma Sufiani, aliiambia STRAIKA kuwa wachezaji walikuwa wanasumbuliwa na uchovu kutokana na mazoezi makali yanayotolewa mfululizo na kocha huyo.
“Ni uchovu tu, Shamte hana tatizo jingine, uchovu unawasumbua wachezaji wetu maana mazoezi haya ni magumu sana,” alisema.
Katika hatua nyingine, baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Saintfiet alitoa adhabu ya kukimbia kuzunguka uwanja kwa muda wa nusu saa kwa wachezaji Salum Telela na Juma Abdul kwa kuchelewa kufika mazoezini leo.
Wawili hao walifika uwanjani hapo saa 3:03 asubuhi ilhali mazoezi ya timu hiyo huanza saa 3:00 asubuhi, hivyo kumkwaza kocha huyo na kuamua kuwaadhibu.
Abdul, ambaye leo ilikuwa ni siku yake ya pili kufanya mazoezi na timu yake hiyo tangu arejee dimbani baada ya kuwa majeruhi, aliungana na Telela, ambaye pia kwa muda mrefu alikuwa majeruhi, kutekeleza adhabu hiyo.
Akizungumza na STRAIKA baada ya mazoezi hayo, Saintfiet alisema hatavumilia utovu wa nidhamu miongoni mwa wachezaji wa timu yake.
Alisema ataendelea kutoa adhabu kwa wachezaji wanaokiuka miiko yao ya kazi na kwamba hatawapanga katika kikosi chake endapo wataendelea kuwa na rekodi za kufanya makosa ya kinidhamu.
“Nidhamu ni kitu cha msingi sana katika timu, mchezaji lazima aheshimu ratiba ya timu. Wachezaji wa Real Madrid, Barcelona na Manchester United wanachelewa mazoezini?” alihoji kwa hasira.
Aidha, kocha huyo alieleza kusikitishwa na taarifa zilizoenea kuwa mshambuliaji wake Jeryson Tegete ameachwa na timu hiyo na anatarajiwa kupelekwa kwa mkopo katika timu ya Toto African ya jijini Mwanza.
Alisema kuwa mchezaji huyo ni mzuri na anacheza kwa ushirikiano na kujituma uwanjani.
“Tegete hakuwa vizuri katika michuano iliyopita ya Kombe la Kagame, lakini hiyo ni hali ya kawaida kwa wachezaji wote duniani. Ni makosa makubwa kwa klabu kumwacha Jery kwa sasa, anajituma na anaonesha kiwango kizuri mazoezini. Naamini ataisaidia timu katika michuano ya ligi kuu msimu ujao,” alisema Saintfiet.
Aidha, kocha msaidizi wa klabu hiyo, Felix Minziro, alifafanua kuwa timu yao iliwasilisha orodha ya wachezaji 28 katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jijini Dar es Salaam juzi kwa ajili ya michuano ya ligi kuu msimu ujao na Tegete ni miongoni mwa wachezaji waliomo katika orodha hiyo.
“Taarifa zinazoenezwa kwa kuwa tuna mpango wa kumpeleka kwa mkopo Tegete katika timu ya Toto ni za uongo na zimelenga kumchanganya mchezaji wetu. Hatuna mpango kama huo,” alisema Minziro.
Yanga wanaendelea na mazoezi hayo kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa michuano ya ligi kuu utakaoanza Septemba Mosi.
Timu hiyo itacheza mechi tatu za kirafiki dhidi ya African Lyon (Jumapili), Coastal Union (Jumatatu) na AFC Leopards ya Kenya (Jumanne).
Labels:
Michezo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment